(+picha) "Jeshi la Baba" Junet, Joho, watokea na nguo mfanano wa kijeshi Kasarani

Junet na Joho ni watetezi wakali wa kinara wa ODM Raila Odinga.

Muhtasari

• Mwanaharakati Boniface Mwangi pia alipakia picha akiwa kwenye nguo sawa na hizo.

Mbunge wa Suna East Junet Mohammed na gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho wakiwa kweney magwanda ya kijeshi
Mbunge wa Suna East Junet Mohammed na gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho wakiwa kweney magwanda ya kijeshi
Image: Junet Mohammed//Twitter

Jumamosi muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulijumuika katika uwanja wa Kasarani wenye uwezo wa kumeza watu takribani elfu 60 katika viti.

Mkutano huu ulikuwa mkubwa zaidi kuadhinimsha siku ya mwisho ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 na matukio mbalimbali yalishuhudiwa ya kufurahisha na mengine ya kuudhi.

Katika moja ya tukio lililozungumziwa zaidi ni pamoja na viongozi wengi wa muungano huo kutokea kwa nguo mfanano ambazo zilikuwa na mshabihiano wa sare za kijeshi vile.

Wengi waliachwa vinywa wazi na picha za viongozi hao zilizosambazwa mitandaoni huku wakisifiwa kwa jinsi walivyotoka kwa kupendeza zaidi na sare hizo zenye nembo ya Azimio la Umoja na nyota tano kwenye upande wa mkono wa kulia na majina ya kila mmoja wao kwenye mnara wa kifuani.

Mbunge wa Suna ya Mashariki Junet Mohammed alipakia msururu wa picha hizo kwenye ukurasa wake wa Twitter wakiwa wametabasamu na gavana anayeondoka wa Mombasa, Ali Hassan Joho na kusema kwamba wako tayari kusimamisha uwanja wa Kasarani.

Baadhi waliwashabikia kwa muonekano fanano huo huku wengine wakiwasuta kwa kile walisema kwamba wanavaa kijeshi kuashiria mapenzi yao kwa vita.

“Ni nini kuvutiwa huku kwa masuala ya kijeshi, vita na ghasia miongoni mwa wanachama wa ODM? Aibu kwenu Joho na Junet,” mmoja kwa jina Leonard Ndirangu aliibua madai hayo.

Wengine waliotoka na fasheni hiyo ni mwanaharakati Boniface Mwangi ambaye kipindi hiki ameonekana kuwa mstari wa mbele kumshabikia Raila Odinga licha ya miaka ya awali kuonekana kutompendelea mwanasiasa huyo kabisa.

Mkutano wa Kasarani ni wa mwisho kwa muungano wa Azimio kuelekea uchaguzi mkuu kulingana na katiba ya Kenya mwaka 2010 inayotaka mikutano rasmi ya kisiasa kukamilika angalau siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Huku hayo yakijiri, muunano pinzani wa Kenya Kwanza nao haukuachwa nyuma kwani walijaza kwa wingi uwanja wa Nyayo jijini Nairobi kwa mionekano maridadi ya fasheni ambayo wingi wao ulikuwa ni rangi ya njano na kibichi kuashiria nembo za muungano huo na haswa chama cha UDA ambacho ndicho mpeperusha bendera William Ruto anatumia kumenyama na Raila kwenye debe Agosti 9.