(+video)“Nimekubali Kenya kuna uhaba wa wapumbavu, wewe ukiwemo" - Matiang'i amchana Ruto

Matiang'i alisisitiza kwamba serikali haitofunga huduma za mitandao ya kijamii na kutaja kauli hizo kama upumbavu.

Muhtasari

• "Mimi sina habari kabisa kuhusu njama yoyote ya kuingilia majukumu ya mamlaka ya mawasiliano nchini CAK, au jitihada yoyote ya kuingilia majukumu ya KPLC kukata umeme" - Matiang'i

Vita vya ubabe kati ya naibu rais William Ruto na Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i vinazidi kuchacha huku Matinag’i sasa akionekana kumkandia Ruto kutokana na madai ambayo yamekuwa yakitoka kwa muungano wake wakisuta baadhi ya idara za serikali kuhusu kuwa na njama ya kutatiza uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ruto na mrengo wake wa Kenya Kwanza wamekuwa wakizilaumu idara za serikali haswa ile inayosimamia usambazaji wa umeme KPLC, IPOA inayosimamia maafisa wa polisi na wizara zingine kama ile ya utandawazi na mawasiliano ICT kuhusu uwepo na njama ya kutatiza uchaguzi kwa kuiba kura kwa niaba ya mpinzani wao mkuu, Raila Odinga.

Matiang’i katika video ambayo aliipakia Ijumaa jioni kwenye ukurasa wake wa Twitter alimsuta vikali naibu rais na wandani wake huku akisema kwamba madai hayo hayana mashiko wala misingi yoyote na katu hayaeleweki mbele nyuma kama kitumbua.

“Ninakubaliana na DP Ruto kwamba Kenya ina uhaba wa wapumbavu, haswa kutoka kwa madai ya kipuuzi ambayo anatoa, na hiyo inatumika zaidi kwa baadhi ya madai madogo yaliyotolewa dhidi ya taasisi zetu zinazotambulika na watu binafsi...Mimi sina habari kabisa kuhusu njama yoyote ya kuingilia majukumu ya mamlaka ya mawasiliano nchini CAK, au jitihada yoyote ya kuingilia majukumu ya KPLC kukata umeme, wakati mwingine katika dunia iliyostaarabika, madai kama haya nayaona kama ni ya kipuuzi kwa mtu kuyafikiria, na wakati yanakuja kutoka kwa viongozi wanaotambulika, unashindwa kujua kama utachela au kulia,” Matiang’i alitema moto kwa kambi ya Kenya Kwanza.

Matiangi alisema kwamba ni jambo la kuonea huruma sana kwa mtu kufikiria kwamba taasisi yenye inajivunia uhuru wa kikatiba kama ile ya mamlaka ya mawasiliano inaweza kuingilia kufanya mambo kama hayo yanayodaiwa kwamba itaingilia uchaguzi.

Waziri huyo alisisitiza kwamba Kenya ni nchi ambayo imekomaa kidemokrasia na hakuna vile serikali itaenda kufunga huduma za kimitandaoni na mitandao ya kijamii kipoindi hiki cha uchaguzi mkuu wiki kesho. Matiang’i aliwataka Wakenya kupuuza kauli kama hizo za DP Ruto huku akizitaja kuwa potofu.