Rais Kenyatta afichua Sababu ya kuwa mstari wa Mbele Kusukuma Mswada wa BBI

"Hakikisha mnawachagua viongozi chini ya mwavuli wa Azimio" - Rais Kenyatta

Muhtasari

• "Mlidanganywa kwamba nilitaka kujiongezea kipindi cha kuhudumu madarakani kupitia mswada wa BBI," - Uhuru Kenyata

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Miezi michache baada ya mahakama ya upeo wa juu zaidi nchini Kenya kutupilia mbali mswada wa marekebisho ya katiba, BBI, sasa rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta amepata kufichua siri ya mswada huo na ni kwa nini alikuwa katika mstari wa mbele kuusukuma ili upitishwe.

Akizungumza katika kaunti ya Murang’a Jumamosi alipokuwa akikagua mradi wa upanuzi wa barabara kuu ya kutoka Kenol kuelekea Sagana na kuishia pande za Marua, rais Kenyatta alionekana kutumia nafasi hiyo kumpigia debe kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga huku akimkandia vikali naibu wake William Ruto kwa kuwaambia watu kwamba Ruto alikuwa anawadanganya eti mswada wa BBI ulinuia kumfanya asalie madarakani.

Rais Kenyatta aliwahakikishia wakaazi wa eneo hilo kwamba wakubali au wakatae Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua watachukua uongozi mapema tarehe 9 Agosti na kuwataka watu wote kujibwaga nyuma yao ili wasiachwe nje.

Rais Kenyatta alifichua kwamba nia yake ya kupigania mswada wa BBI haikuwa kumrefushia kipindi chake cha kuhudumu madarakani kama baadhi ya viongozi walivyokuwa wakisema bali alikuwa na nia njema ya kuhakikisha kwamba watu wa eneo la Mlima Kenya lenye idadi ya watu wengi lingefaidi zaidi kutokana na idadi yake kuliko sehemu zingine zisizo na idadi sawqa na eneo hilo.

“Niamini mimi au mkatae, mchezo huu utashindwa na Raila Odinga na Martha Karua. Hakikisha mnawachagua viongozi chini ya mwavuli wa Azimio…mlidanganywa kwamba nilitaka kujiongezea kipindi cha kuhudumu madarakani kupitia mswada wa BBI, ila tulichokuwa tukikitaka ni eneo pana la Mlima Kenya lenye wingi wa watu kufaidi usawa wa mapato ya taifa kuliko sehemu zingine za nchi zenye uchache wa watu,” rais Kenyatta alisema.

Itakumbukwa shirika la Linda Katiba likiongozwa na Martha Karua ambaye sasa rais Kenyatta anampigia debe ndilo lilikuwa mstari wa mbele mahakamani kupinga mswada huo wa BBI ambao uliangushwa katika mahakama zote kutoka mahakama kuu, mahakama ya rufaa na hata mahakama ya upeo wa juu zaidi nchini.