(+video) DP Ruto atimuka mbio kwa miguu kutoka Nyayo kuenda Wilson kuwahi ndege

Ruto alienda moja kwa moja hadi Uwanja wa Ndege wa Wilson kutoka uwanja wa Nyayo kwa mkutano wa mwisho Kiambu...

Muhtasari

• Mikutano ya Jumamosi ilifikisha mwisho wa kipindi cha kampeni kwa mujibu wa sheria na ratiba za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Jumamosi ilikuwa siku yenye pilka pilka na heka heka nyingi miongoni mwa wanasiasa mbalimbali nchini waliokuwa wakihaha kutoka sehemu moja kuelekea ingine kuhakikisha wamerindima ngoma zao siku hiyo ikiwa ndio funga-kazi kwa kampeni rasmi nchini kuelekea uchaguzi mkuu.

Naibu Rais William Ruto pia hakuachwa nyuma kwani baada ya mkutano mkuu katika uwanja wa Nyayo, alitoka mbio tena kwa miguu bila kujali kusubiri hata walinzi wake, na akaelekea moja kwa moja kwa haraka mno katika anga tua ya Wilson ili kuabiri ndege kumpeleka eneo la Kiambu alikokuwa na nia ya kuwahutubia wakaazi wa kaunti hiyo yambapo ni ya pili kwa kura nyingi nchini baada ya Nairobi.

Muungano wa Kenya Kwanza ulikuwa ufunge kampeni zake katika uwanja wa Kiambu wa Kirigiti.

Sheria ya Uchaguzi inawataka wagombea kufanya mikutano yao ya mwisho ya kampeni saa 48 hadi siku ya kupiga kura. Muda wa mwisho ulikuwa unakamilika saa kumi na mbili jioni na ndio maana Ruto alikuwa anakimbia angalau kujipigia debe kwa mara ya mwisho kabisa kabla ya makataa kubisha.

Katika video iliyosambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii, DP anaonekana akikimbia kando ya barabara ya kurukia ndege huku akikimbilia kwenye chopa inayosubiri, pamoja na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Ilikuwa siku yenye shughuli nyingi kwa DP ambaye mapema siku hiyo aliongoza mkutano wa Kenya Kwanza katika mkutano na wanahabari huko Karen, kabla ya kuelekea kaunti ya Narok.

Msafara wa Kenya Kwanza kisha ulirejea Nairobi hadi uwanja wa Nyayo kwa mkutano mkuu.

Wengi wamemzoea naibu rais William Ruto kuwa na siku iliyoshikika na kubanana na ziara nyingi mno ambapo anaweza akazunguka kaunti zaidi ya sita kote nchini chini ya siku moja, kuzinadi sera za muungano wa Kenya Kwanza.