Afisa wa IEBC amekamatwa na polisi baada ya kupatikana na karatasi za kupigia kura nyumbani kwake.
Afisa wa uchaguzi katika kaunti ndogo ya Webuye Mashariki, Emmanuel Onyango alisema afisa huyo alikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wakazi wa Maraka huko Webuye, kaunti ya Bungoma.
"Polisi wa eneo hilo walifanikiwa kumkamata mmoja wa maafisa waliorejea, ambaye alipatikana akiwa na karatasi za kupigia kura katika makazi yake. Tumemkamata na yuko chini ya ulinzi wa polisi," Onyango alisema.
Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ndogo aliongeza kuwa maafisa wengine wawili wa uchaguzi bado wako mbioni lakini polisi wanaendelea kuwafuatilia.
Akihutubia wanahabari, Onyango aliongeza kuwa karatasi hizo zilipaswa kuwa katika kituo cha kupigia kura.
"Ni kinyume cha katiba na ni kinyume cha sheria kuwa na nyenzo zozote za uchaguzi majumbani mwenu," aliongeza.
Martin Wanyonyi Pepela, mgombeaji, ambaye anahusishwa na tukio hilo alikanusha madai hayo.
Wanyonyi amewahakikishia washindani wake kutokuwa na shaka kuhusu uaminifu wa IEBC katika kutoa matokeo ya haki.
Wagombea tofauti wa kisiasa kutoka eneo hilo wameibua wasi wasi wao kuhusu utayarifu wa IEBC katika kuhakikisha uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.
Haya yanajiri baada ya karatasi za kupigia kura za kiti cha ugavana kaunti ya Kirinyaga kugunduliwa katika kaunti ndogo ya Mumias Mashariki, kaunti ya Kakamega.
Msimamizi wa eneo hilo, Joseph Ayatta alithibitisha kisa hicho.
Ripoti zinaonyesha kuwa kulikuwa na mkanganyiko katika usambazaji wa karatasi za kupigia kura.
Imetafsiriwa na MOSES SAGWE