Jumatatu imekuwa siku yenye pulkapilka si haba huku vifaa vya kupiga kura vikisafirishwa katika kila kituo cha kupiga kura mbele ya uchaguzi mkuu Jumanne Agosti 9.
Katika kaunti ya Mombasa, kulishuhudiwa mkanganyiko na kizaazaa baada ya karatasi za kupiga kura za wagombea wa ugavana amabazo zilifaa kupelekwa eneo bunge la Mvita kukosekana na badala yake zile za kaunti ya Kilifi kupelekwa huko
Akizungumza katika shule ya upili ya Allidina Visram kilichopo kwenye kaunti hiyo wakati wa kusimamia ufunguzi na usambazaji wa karatasi za kupiga kura, Masha Sudi ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mvita alikiri kuwepo kwa mkanganyiko huo na kusema wanalifanyia kazi suala hilo ili kulitatua kwa wakati.
"Tumepokea karatasi za kupigia kura Kilifi. Hata hivyo, hiyo ni changamoto ambayo tunaweza kufikia na tutaisuluhisha hivi karibuni," Sudi alisema.
Kuhusu mkanganyiko uliosababishwa na kukosekana kwa karatasi za kupigia kura, Sudi alisema ameshafikisha mawasiliano kwenye mamlaka husika na hatua zimeanza kushughulikia tatizo hilo.
“Natoa wito kwa wakazi wa Mombasa kuwa watulivu na wawe na uhakika kwamba kesho asubuhi watampigia kura mgombeaji wa ugavana wanayempendelea,” akasema.
Zaidi ya hayo, aliwataka watu kuacha uvumi kuhusu karatasi za kupigia kura za mgombea ugavana zilipo.
Alisema uvumi wowote ni uongo kwani hakuna anayejua zilipo mpaka kipindi hicho cha mkanganyiko huo.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi alisema tatizo hilo linaweza kuwa ni ufungashaji wa vifaa nje ya nchi, ambapo zoezi hilo lilifanyika na kufungwa.
"Tulipokea zikiwa zimefungiwa na kuzifungua kwa mara ya kwanza, mbele ya watu na vyombo vya habari. Unajua hao ni Wazungu na labda walidhani Kilifi na Mombasa ni kitu kimoja," alisema.
Alisema siku ya Jumanne vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na zoezi la upigaji kura litaanza hadi saa kumi na moja asubuhi.
Hata hivyo, aliongeza, iwapo kutakuwa na watu kwenye foleni saa kumi na moja jioni, basi wataruhusiwa kupiga kura zao.
Ni wale ambao watakuja baada ya saa kumi na moja jioni ambao hawataruhusiwa kupiga kura.