Wafahamu wagombea watatu wanaosubiri kuapishwa tu

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema watatu hao wataapishwa baada ya uchaguzi.

Muhtasari

•Chebukati alisema watatu hao wataapishwa baada ya uchaguzi kwa sababu hakuna aliyejiandikisha kuwapinga kwenye kura.

•Kukosekana kwa washindani kwa wagombea hao watatu kulifanya iwe rahisi kwao kusalia washindi kabla ya siku ya kupiga kura.

Naibu Rais William Ruto na mgombeaji wa Uwakilishi wa Kike wa UDA Kericho Beatrice Kemei.
Naibu Rais William Ruto na mgombeaji wa Uwakilishi wa Kike wa UDA Kericho Beatrice Kemei.
Image: FELIX KIPKEMOI

Wagombea watatu wamepata ushindi wa moja kwa moja na wanasubiri kutangazwa washindi na tume  la uchaguzi na mipaka nchini kabla ya kuapishwa.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema watatu hao wataapishwa baada ya uchaguzi kwa sababu hakuna aliyejiandikisha kuwapinga kwenye kura.

Watatu hao ni pamoja na mgombea mwakilishi wa wanawake wa Kericho Beatrice Kemei, Issa Aden alinyakua kiti cha MCA wa Wadi ya Sabena huko Lagdera, Kaunti ya Garissa na Julius Kimutai  ambaye ataapishwa kuwa MCA wa Wadi ya Ravine katika eneo bunge la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo.

Kemei na Kimutai wanatoka chama cha United Democratic Alliance (UDA) huku Aden akitoka chama cha National Agenda.

Maelfu ya wagombea viti wamekuwa wakijipigia debe katika juhudi za kuchukua uongozi kabla ya uchaguzi wa Jumanne.

Kukosekana kwa washindani kwa wagombea hao watatu kulifanya iwe rahisi kwao kusalia washindi kabla ya siku ya kupiga kura.

Chebukati alikuwa amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la milioni 2.6 la idadi ya wapiga kura waliohitimu nchini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Ukiangalia kiwango cha uandikishaji, mwaka wa 2017 waliosajiliwa wapiga kura na IEBC ikilinganishwa na waliohitimu na KNBS waliwakilisha asilimia 77.78 na 2022 inawakilisha asilimia 79.41," Chebukati alisema.

Chebukati pia alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 13.08 la vituo vya kupigia kura kati ya chaguzi kuu mbili.

"Mwaka wa 2017, tulikuwa na vituo 40,883 vya kupigia kura, kwa 2022 tuna vituo 46,232," Chebukati alisema.

(Utafsiri: Samuel Maina)