Mgombea mwenza wa urais wa William Ruto, Rigathi Gachagua amekuwa mtu wa kwanza kufaidi kutoka kwa matumizi ya sajili ya kupiga kura iliyochapishwa baada ya jina lake kukosekana katika sajili ya kidijitali.
Gachagua alirauka katika kituo cha kupiga kura ambapo jina lake liitafutwa kwenye sajili ya kidijitali na kukosekana na ikalazimika kutumia sajili mbadala iliyochapishwa ili kupiga kura yake.
“Nimefurahia sana kwa wakenya wengi waliojitokeza kupanga foleni kuwachagua viongozi vyake. Ninataka kuwaomba Wakenya wote kujitokeza kupiga kura, kudumisha amani na kuwachagua viongozi wanaowataka,” Alisema Rigathi Gachagua.
Gachagua ambaye ni mgombea mwenza wa Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza anakuwa mtu wa kwanza kabisa mashuhuri kufaidi kutoka kwa sajili iliyochapishwa licha ya chama chao cha UDA kuelekea katika mahakamani ya rufaa Jumatatu kupinga agizo lililotolewa na mahakama ya juu kutaka sajili iliyochapishwa kutumiwa.
Mahakama ya rufaa ilitoa uamuzi wa kutupilia mbali agizo hilo la mahakama ya juu na kusema sajili iliyochapishwa haitatumika kimsingi isipokuwa tu pale ambapo vifaa vya kidijitali vya KIEMS vimefeli.
Mwenyekiti wa IEBC alipokea uamuzi huo uliotolewa Jumatatu jioni na kusema kwamba tume hiyo itajitahidi kutii agizo la mahakama na kwamba itatumika sajili iliyochapishwa kama mbadala wakati sajili ya kidijitali kwenye mitambo ya KIEMS imefeli, ingawa alisema hawatarajii mitambo hiyo kufeli.
Huku hayo yakijiri, mtambo wa KIEMS katika eneo bunge la Nyali umeripotiwa kufeli kufanya kazi na kulazimu matumizi ya sajili iliyochapishwa.