Miezi mitano baada ya kutangaza kuwa anastaafu kutoka siasani, Gavana wa Isiolo Mohamed Kuti alipiga kura Jumanne akiwa kwa kiti cha magurudumu.
Akiwa ameketi kwenye kiti, alisukumwa kwenye kituo cha kupigia kura na kupelekwa kwenye chumba cha kupigia kura.
Alikuwa na plasta kwenye mguu wake wa kulia huku upande wa kushoto akiwa na buti ya kutembea.
Mnamo Aprili mwaka huu, Kuti aliachana na azma yake ya kuchaguliwa tena, akitoa sababu ya afya mbaya. Hakufafanua. Amekuwa mgonjwa tangu Desemba mwaka jana.
Wakati akitangaza kustaafu kwake kutoka kwa siasa kali, Kuti aliidhinisha kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Nairobi Abdi Guyo kumrithi.
"Kwa bahati mbaya, hivi majuzi nimepata changamoto za kiafya ili nihisi kuwa ni wakati wa kukabidhi uongozi kwa jamii yangu ya Sakuye na kaunti ya Isiolo kwa jumla," alisema.
"Ninawashukuru watu wa Isiolo ambao wameniunga mkono kwa miaka 20 iliyopita na pia ambao nimehudumu kama afisa wa matibabu kwa miaka 10 na miaka 20 katika siasa," gavana huyo aliongeza wakati huo huo.
"Nimetoa wito kwa jamii yangu kuunga mkono MCA wa Spring Valley/Matopeni Abdi Guyo," Kuti alisema. Guyo alikuwa chaguo la jamii, alisema.
Gavana huyo mwenye umri wa miaka 58 amekuwa katika siasa kali kwa miaka 20, akihudumu kama mbunge wa Isiolo Kaskazini kwa mihula miwili na muhula mmoja kama seneta.
Alihudumu kama waziri msaidizi wa Afya kati ya 2004 na 2005, Waziri wa Masuala ya Vijana mwaka 2005 na Waziri wa Mifugo kutoka 2008 hadi 2013 wakati wa Rais wa zamani Mwai Kibaki.
Tafsiri na MOSES SAGWE