Mgombea urais kutoka mrengo wa Kenya Kwanza ambaye ndiye Naibu Rais anayeondoka, William Ruto sasa anapumzika katika boma lake yla kifahari huko Sugoi saa chache baada ya kupiga kura yake asubuhi ya Jumanne, Agosti 9.
Ruto alikuwa mpiga kura wa kwanza katika Shule ya Msingi ya Kosachei, ambapo aliandamana na mkewe Rachel Ruto na walifika saa kumi na mbili asubuhi.
Kinyume na wengi waliotarajia kwamba Ruto angeabiri helikopita yake na kurudi Nairobi katika makazi rasmi ya naibu rais huko Karen, aliamua kusalia Sugoi ili kustarehe huku upigaji kura ukiendelea kote nchini.
Katika picha ilipakiwa na mbunge anayeondoka wa Soy Caleb Kositany, Ruto alifurahia mwanga wa jua akiwa amestarehe na mbunge huyo huku kando yake kukiwa na meza yenye kikombe cheney kinywaji moto amabcho kinakisiwa kuwa chai.
Kositany katika picha hiyo aliyoipakia Twitter, aliifuatisha kwa maneno kwamba ‘Kuchunga Amani’
Katika wadhifa mwingine wa mgombea Ugavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii-Chelilim almaarufu Koti Moja, Ruto na mkewe pia walipokea wageni waliomtakia heri shughuli za uchaguzi zikiendelea.
"Nimemtembelea Rais wetu wa 5, Mheshimiwa William Samoei Ruto, nyumbani kwake Sugoi wakati mchakato wa upigaji kura wa amani ukiendelea kote nchini. Nimetuma salamu zangu kwa Rais wetu anayekuja na kumtakia kila la kheri tunapotarajia kukamilika kwa uchaguzi mkuu kote nchini,” Koti Moja alisema.
Koti Moja analenga kuwa mrithi wa gavana Jackson Mandago katika kaunti hiyo ambayo ndio kitovu cha Bonde la Ufa huku mpinzani wake mkuu akiwa mfanyibiashara Zedikiah Bezeki Bundokich.
Gavana Mandago anawania kuwa seneta kwa tikiti ya chama cha UDA.