Uchaguzi mkuu unapoendelea kote nchini Kenya, katika kaunti ya Kisii hali ni tete baada ya maandamano makali kukumba eneo bunge la Bonchari baada ya mtu aliyesemekana kujihami kwa bunduki kumpiga risasi na kumjeruhi vibaya mpiga kura mmoja kufuatia kutofautiana naye kisiasa.
Wakaazi walisema mzozo kuhusu utiifu wa kisiasa kwa baadhi ya wagombea ulizusha ufyatulianaji wa risasi kwenye eneo la Bosiabano nje ya mji wa Suneka usiku.
Kulikuwa na maelezo machache juu ya utambulisho wa mpiga risasi huyo ingawa baadhi ya wakaazi walisema ni mmoja wa maaskari wa eneo hilo.
Mwathiriwa alipata majeraha kwenye tumbo.
Kamanda wa Kaunti Ndogo ya Gesonso Charles Machinji alisema tayari wamemkamata mshukiwa mkuu aliyetumia bunduki vibaya kumjeruhi mtu.
“Tayari tumeanza uchunguzi na tutatoa maelezo zaidi kadri yanavyoendelea,” alisema.
Visa kama hivyo vinatokea wakati ambapo katika eneo bunge la Ugenya pia milio ya risasi ilitatiza uchaguzi baada ya watu wanaoegemea upande wa mgombea mmoja kumpiga na kumjueruhi naibu chifu wa eneo hilo kwa kile waliteta kwamba uwepo wake katika kituo hicho cha kupiga kura utatatiza upigaji kura.
Visa vingine vya msukosuko vilishuhudiwa usiku wa kuamkia leo katika kaunti ya Wajir kulingana na video iliyosambazwa mitandaoni ikionesha wananchi wakikimbilia maisha yao baada ya milio ya risasi kusikika katika ukumbi wa kituo cha kupiga kura cha Eldas.