Uchaguzi mkuu katika nyadhifa mbalimbali nchini ukiwa unaendelea na baadhi ya sehemu kukiripotiwa matatizo ya vifaa vya kupiga kura, kweney kaunti ya Nandi Hills, karatasi za kupiga kura za wajumbe wa kaunti, MCAs zimepotea kwa njia tatanishi.
Karatasi hizo zinasemekana kutoweka katika njia isiyoeleweka kutoka chumba kimoja ambacho karatasi hizo zilikuwa zimewekwa katika kituo cha kupiga kura cha shule ya msingi ya Our Lady of Peace
Baada ya kupotea kwa karatasi hizo, maafisa wa tume huru ya mipaka na uchaguzi ya IEBC waliwasihi wananchi kendelea kupiga kura katika nyadhifa nyingine huku karatasi hizo za kupiga kura za wajumbe wa kaunti zilitafutiwa ufumbuzi wa kupotea kwao.
Afisa aliyehutubia wakazi alisema upigaji kura wa MCA utaghairiwa kabisa, kwa kituo hicho.
"Tumekubaliana karatasi za kupigia kura za MCA kwa chumba kimoja, zirudishwe kwenye kituo tupu. Itahesabiwa kuwa tupu," alisema.
Afisa huyo hata hivyo amewataka wapiga kura kudumisha amani ili shughuli hiyo iendelee vizuri.
Haya yanajiri huku ikiripotiwa kwamba mtambo wa kidijitali wa KIEMS ukipotea katika kaunti ya Marsabit kisa ambacho mwenyekiti wa tume ya IEBC alidhibitisha na kusema kwamba tayari mtambo huo ushazimwa kabisa na kubadilishwa.