(+video) Raila apokelewa Kishujaa kituo cha kupiga kura cha Old Kibra

Raila aliwasili katika kituo hicho huku akilakiwa na mamia ya wafuasi wake waliomsubiri kwa mbwembwe tele

Muhtasari

• Raila alifika katika kituo cha kupigia kura dakika chache hadi 10.30 asubuhi. Alikuwa ameandamana na mkewe Mama Ida Odinga.

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga akipiga kura katika kituo cha shule ya msingi ya Old Kibera mnamo Agosti 9, 2022.
Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga akipiga kura katika kituo cha shule ya msingi ya Old Kibera mnamo Agosti 9, 2022.
Image: THE STAR//ENOS TECHE

Mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amewasili katika shule ya msingi ya Old Kibra ambayo ndio kituo chake cha kupiga kura.

Raila ambaye ni mmoja kati ya wagombea wanne wa uchaguzi wa urais mwaka 2022 amekuwa wa mwisho kupiga kura yake baada ya awali wagombea wengine kama William Ruto wa UDA akiwa wa kwanza kupiga kura yake eneo la Sugoi, David Mwaure wa Agano alipiga kura yake pia maeneo ya Upperhill Nairobi akifuatiwa na wakili msomi George Wajackoyah ambaye alifika maeneo ya Matungu dakika chache tu mbele ya Odinga na mtambo wa KIEMS ukafeli kumfanya asubiri kwa muda zaidi ili kuona kama atapiga kura.

Raila aliwasili katika kituo hicho huku akilakiwa na mamia ya wafuasi wake waliomsubiri kwa mbwembwe tele kumkaribisha Old Kibra.

"Tumefanya tuwezavyo katika suala la kampeni. Sasa mpira uko kwenye mahakama ya watu na nina imani watu wa Kenya watazungumza kwa sauti kubwa kuunga mkono mabadiliko ya kidemokrasia," alisema huku umati usiochoka ukimshangilia na kumsindikiza nje ya shule ya msingi ya Old Kibra.

Raila alifika katika kituo cha kupigia kura dakika chache hadi 10.30 asubuhi. Alikuwa ameandamana na mkewe Mama Ida Odinga.

Mgombea mwenza wake Martha Karua alikuwa mtu wa kwanza kupiga kura katika kituo cha Mugumo huko Gichugu mnamo Jumanne saa kumi na mbili asubuhi.