Watu Wanne wajeruhiwa katika mzozo wa vita kati ya wagombea ubunge Bumula

Mabanga anadaiwa kufyatua risasi waziwazi gari la Wamboka wakati wa kisa hicho cha saa tatu asubuhi

Muhtasari

• Tukio hilo la saa tisa asubuhi lilishuhudia magari manne yakipigwa risasi na kugongana huku waathiriwa wakijaribu kukwepa mzozo huo.

• Kisa hicho kiliwaacha watu wanne kujeruhiwa na hali mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma.

USHINDANO WA KISIASA: Moja ya magari yaliyoharibiwa wakati wa mzozo kati ya Jack Wamboka wa DAP-K na Mwambu Mabanga wa UDA lilikabiliana usiku.
USHINDANO WA KISIASA: Moja ya magari yaliyoharibiwa wakati wa mzozo kati ya Jack Wamboka wa DAP-K na Mwambu Mabanga wa UDA lilikabiliana usiku.
Image: TONY WAFULA

Usiku wa kuamkia Jumanne Agosti 9 wakenya wakirajiwa kurauka kuwachagua viongozi wao, katika eneo bunge la Bumula hali ilikuwa tete baada ya wagombea ubunge kutoka vyama viwili hasimu kumenyana na kujeruhiana.

Wagombea hao ni Jack Wamboka kutoka chama kipya kabisa cha DAP-K na Mwambu Mabanga kutoka chama cha UDA walianza kurushiana cheche baada ya kudaiwa kwamba Mabanga wa UDA alifyatua risasi kwa gari la Wamboka, jambo lililozua mtafaruku.

Kisa hicho kiliwaacha watu wanne kujeruhiwa na hali mahututi katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Bungoma.

Katika mkasa huo uliotokea usiku, mwalimu mkuu aliyetambuliwa kama Walter Wanjala alikuwa miongoni mwa wanne waliojeruhiwa wakiwemo jamaa wengine waliotambuliwa kwa majina Joseph Wanyonyi, Simon Mayende, Munishi na Hesbon na wengine watatu waliohusika katika mtagusano huo wakiwa bado hawajapatikana

Kisa hicho cha saa tisa alfajiri kilishuhudia magari manne yakipigwa risasi na kugongana huku waathiriwa wakijaribu kukwepa kutoka tukio hilo la kisiasa.

Haijajulikana wanasiasa hao walikuwa wakifanya nini majira ya usiku mpevu kama huo kwani tayari muda rasmi wa kufanyika kampeni ulikamilika siku mbili zilizopita kuambatana na matakwa ya katiba ya mwaka 2010 inayotoa makataa ya kukamilika kwa kampeni angalau saa 48 kabla ya siku rasmi ya uchaguzi.

Hayo yanajiri huku uchaguzi wa ugavana katika kaunti Jirani ya Kakamega ukiwa umesitishwa na tume ya IEBC kufuatia mkanganyiko wa karatasi hizo ambao ulitokea Jumatatu baada ya karatasi ambazo hazikuwa za kaunti hiyo kusambazwa kuelekea eneo hilo lenye wapiga kura wengi katika mkoa wa Magharibi.