Wakili maarufu Cliff Ombeta amekubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha ubunge wa eneo la Bonchari.
Kupitia taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter, Ombeta alielezea kuridhishwa kwake na safari yake ya kuwania ubunge na uzoefu aliopata.
"Bonchari ilikuwa na maono tofauti na yangu. Nashukuru kwa mbio na uzoefu. Labda wakati mwingine tutakuwa na mtazamo sawa," Ombeta alisema Jumatano asubuhi.
Amekuwa mgombea wa tatu kukubali kushindwa hadharani katika kinyang'anyiro cha mwaka huu. Wengine waliokubali kushindwa ni Moses Kuria ambaye alikuwa anawania ugavana Kiambu na mbunge wa Taveta Naomi Shaban.
Ombeta hata hivyo alidokeza kuwa kushindwa kwake katika kinyang'anyiro sio mwisho wa azma yake ya kisiasa.
"Bonchari Enyia imekuwa na itaendelea kuwa moyoni mwangu. Walioniamini, tutaiweka hai. Huu hautakuwa mwisho wetu kisiasa," Ombeta alisema.
Wakili huyo aliishukuru timu yake ya kampeni na kuwataka kuweka roho hai hata kama alikiri kuwa maono yake yalitofautiana na yale ya wapiga kura wa Bonchari ambao alitaka kuwakilisha katika uchaguzi mwaka huu.
Ombeta alikuwa akiwania ubunge wa Bonchari kwa tikiti ya chama cha UDA dhidi ya wagombeaji wengine 11.
Miongoni mwao ni pamoja na mbunge wa sasa Pavel Oimeke na waliokuwa wabunge Mary Otara na Zebedeo Opore wa Green Movement Party na Jubilee Party mtawalia.
Wengine ni Kevin Mosomi wa Party of Democracy and Unity (PDU), Victor Omanwa wa Party of Economic Democracy (PED), Jonah Ondieki wa The New Democrats (TND). Eric Oigo wa National Reconstruction Alliance (NRA), David Ogega wa Kenya Social Congress (KSC), Margaret Nyabuto wa Maendeleo Chap Chap (MCC), Charles Mogaka wa Progressive Party of Kenya (PPK), Paul Matagaro wa Mwangaza Tu Party na Jeremiah Atancha wa Agano Party nao walikuwa kwenye kinyang'anyiro hicho
Hapo awali mbunge wa Taveta Naomi Shaban ambaye amekuwa akihudumu kwa muda mrefu alikubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha mwaka huu.
Naomi ambaye alikuwa anatazamia kuchaguliwa kwa muhula wa tano aliwaambia wafuasi wake kwamba matokeo ya awali yalionyesha kwamba hatanyakua kiti hicho.
"Asante kwa kunipa nafasi ya kukuhudumia kwa miaka 20. Ndugu yangu mdogo Okano, nakupongeza," aliandika katika kundi la WhatsApp.
Naomi ambaye alijiunga na siasa mwaka wa 2002 ni mmoja wa wabunge waliokaa muda mrefu zaidi eneo la Pwani. Amehudumu kama mbunge kwa miaka 20 baada ya kumng'oa aliyekuwa mbunge Basil Criticos.