Jamii ya Washona wapiga kura kwa mara ya kwanza

Mnamo 2020, Uhuru alitoa uraia kamili wa Kenya kwa watu 1,670 kutoka kwa jamii hiyo

Muhtasari

• Washona walikuwa hawajapewa uraia kamili nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 50.

• Jamii ya Wasona waliwasili nchini kutoka Zimbabwe katika miaka ya 1950 kama wamisionari.

Jamii ya Shona wakisherehekea wakati wa mkutano na wanahabari kwa kuonyesha vitambulisho vyao.
Jamii ya Shona wakisherehekea wakati wa mkutano na wanahabari kwa kuonyesha vitambulisho vyao.
Image: Star

Jamii ya Washona wamepiga kura zao kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50 ya kutokuwa na utaifa.

Mnamo 2020, Rais Uhuru Kenyatta alitoa uraia wa Kenya kwa watu 1,670 kutoka jamii ya Washona na Wanyarwanda 1,300, ambayo inawaruhusu haki ya kupiga kura.

Christopher Samson, ambaye ni mwanachama wa jamii ya Washona, alisema juhudi za kutafuta msaada kutoka kwa serikali zilizopita hazikufaulu.

“Dua zetu za muda mrefu zimesikika. Tumehangaika sana, tumepoteza fursa nyingi na mali nyingi kwa vile hatuna utaifa," Samson alisema.

Wanachama wa Shona walikuwa miongoni ya wapiga kura zaidi ya milioni 22 waliojiandikisha, ambao walijitokeza Jumanne kupiga kura.

Wanawake na watoto walikuwa wamevalia mavazi meupe walipokuwa wakienda kupiga kura zao.

Jamii hiyo inayoishi Kinoo, kaunti ya Kiambu, ilitambuliwa kama kabila la 46.

Uamuzi huo uliofanywa na Rais uliitwa "maendeleo ya kubadilisha maisha kwa maelfu ya watu" na UNHCR.

Jamii ya Washona iliwasili kutoka Zimbabwe hadi nchini katika miaka ya 1950 kama wamisionari.

MCA wa Kinoo Samuel Kimani alisema kuwa zaidi ya wanachama 3,500 wa Washona wamepokea vyeti vya kuzaliwa.