"Mshindani wangu Jalang'o Anaongoza na Nampongeza" Mbunge Nixon Korir wa Lang'ata

Korir alichaguliwa kama mbunge wa eneo hilo mnamo 2017 kupitia tikiti ya chama cha Jubilee

Muhtasari

Siasa si chuki. Mungu ambariki Langata - Korir

Mbunge wa Lang'ata Generali Nixon Korir akikubali kushindwa ubunge
Mbunge wa Lang'ata Generali Nixon Korir akikubali kushindwa ubunge
Image: Nixon Koriri//Facebook

Mbunge wa Lang’ata jijini Nairobi Jenerali Nixon Korir amekuwa mwanasiasa mwingine wa hivi karibuni tena kutoka mrengo wa naibu rais William Ruto, Kenya Kwanza kukubali matokeo baada ya kushindwa kukitetea kiti chake katika eneo bunge hilo.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Korir aliwashukuru wakaazi wa Lang’ata kwa kumpa nafasi ya kuwahudumia bungeni na pia amemhongera mshindani wake wa karibu Phelix Odiwuor, mchekeshaji na mtangazaji maarufu kwa jina Jalang’o.

“Kwa wananchi wa Langata, ninawashukuru kwa dhati kwa kunipa nafasi ya kuwa Mbunge wenu kwa miaka 5 iliyopita. Imekuwa ni fursa nzuri ambayo ilinipa nafasi ya kuchangia ujenzi wa taifa letu na huduma kwa watu. Kutokana na matokeo ambayo tumejumlisha katika kituo cha Generali, mshindani wangu Jalango anaongoza na ninataka kumpongeza anapojiandaa kutwaa taji hilo na kuisogeza mbele Langata. Siasa si chuki. Mungu ambariki Langata,” Korir aliandika.

Taarifa za Korir kukubali matokeo mapema zinakuja saa chache tu baada ya wenzake kutoka kambi ya Kenya Kwanza wakiwemo mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliyekuwa akiwania ugavana Kiambu kwa tikiti ya Chama Cha Kazi, Wakili Cliff Ombeta aliyekuwa akiwania ubunge Bonchari kwa tikiti ya UDA, George Theuri wa Embakasi Magharibi aliyeuwa akiwania ubunge wa tikiti ya UDA  miongoni mwa wengine kutangaza kukubali kushindwa na kuwatakia kila la kheri washindani wao.