Wananchi wana haki kidemokrasia na kikatiba kuwateua viongozi katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.Ni fursa murwa waliokirimiwa kufanya mabadiliko kwa faida ya jamii zao.
Bara la Afrika kwa muda mrefu limetingwa na changamoto si haba licha ya hatua au mikakati kuwekwa ili kubadilisha hali mbaya.Utovu wa tabia na uongozi uliozorota umekuwa dondandugu tangu mkoloni kufunganya virago vyake.Kiongozi anayeshikilia uongozi ni zaidi ya hayawani.
Siasa za mtu mweusi zimehusishwa na kashfa, cheche na mgawanyiko katika misingi ya kikabila.Vita baina ya jamii hasa husababishwa na tofauti za kisiasa na ugavi wa raslimali. Jamii zenye idadi kubwa ya wapiga kura wakitaka kujinufaisha pakubwa huku wengine wakizama kwenye lindi la akina pangu pakavu.
Taifa la Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo kwa takaribani miongo sita bado saisa zao ni zile za ‘nitafanya hiki na kile’ almradi mwanasiasa ashinde katika kinya’nga’nyiro.Vitu vya kimsingi bado ni shida kwa wananchi kuvimudu. Ni dhahiri kwamba bado jamii halijaamua linahitaji nini na kulifanyia kazi kwa madhumuni ya kutimiza ndoto zao.
Nchi ya Uswizi [ Sweden] ni kati ya mataifa ambazo raia wake hawakumbani na tatizo la uhaba wa maji, chakula, afya na lishe bora. Hii ni kwa sababu waliopewa uongozi walifahamu jukumu lao na daima hawakuchelea kutekeleza miradi endelevu. Hii ina maana hamna ufisadi katika nchi hii na zile zingine zilizopiga hatua mbele kimaendeleo?
Tofauti na hulka za mwafrika, viongozi katika mataifa kama vile Sweden, Ujerumani, Amerika na zingine wamejizatiti zaidi kutumia asilimia kubwa ya hela zilizotengewa afisi zao katilka kutekeleza maendeleo.
Kulingana na Joseph Nyasani na Michael Todaro ambao ni wataalam wa maswala ya jamii na maendeleo,wawili hawa wanakubaliana katika tafiti zao kwamba mwafrika hutumia karibu kila kitu kuhudumia tumbo na familia zao pasi kujali raia wanaotegemea hudumu za serikali
Serikali ya Jubilee inayoondoka mamlakani baada ya kura za uchaguzi, ilijishughulisha pakubwa katika kuboresha miundomsingi kama vile barabara, daraja, miradi ya maji miongon i mwa zingine.Hii huchangia katika maendeleo ya jamii katika kila sekta.
Lakini Profesa Nyasani, katika tafiti zake katika mbinu za kustawisha Kenya, anasema kujenga barabara na miundomsingi zingine si tosha wakati wakazi wanalala njaa. Anaelezea kuwa uzalishaji wa chakula na wananchi kuwa na uhuru kubadilisha hali na maisha yao ndo inayowapa furaha.
Katika kampeni za wagombea kiti cha urais kutoka muugano wa Azimio la umoja one- Kenya[Raila Odinga], Kenya Kwanza[William Ruto], chama cha Agano[ David Mwaure], na Roots Party[Prof Wajackoyah], vyote vilishamiri ahadi za kuboresha uchumi na kutengeneza nafasi zaidi za ajira kwa vijana.
Kinachowapa wakenya kiwewe ni kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa ahadi za uongo. Kwa mfano zaidi ya asilimia 35 ya wanafunzi kutoka vyuo vya kiufundi na vikuu hawakuripoti shuleni kwa sababu za ukosefu wa karo na pesa kumudu mhitaji mengine.
Takwimu zaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 23.7 hawana uwezo wa kukidhi mahitaji yao. Ukosefu wa lishe na afya bora ikichangia katika idadi ya ugonjwa wa utapiamlo na vifo.Hawa watu takribani million ishirini wanahitaji kukomolewa toka kwenye jinamizi linalowasibu haraka iwezekanavyo.
Kuna haja ya taifa hili kujifunza kutoka kwa mataifa kama vile Uchina yaliyopiga hatua mbele kimaendeleo. Uchina imeweza kuwakomboa watu kuzidi milioni 800 kutoka kwenye umasikini. Sera na utekelezwaji wa miradi ulishabikiwa na raia wengi ambao hali yao ilikuwa heri ya jana. Leo hii taifa la China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji na teknologia.
Kenya ina uwezo wa kujitegemea ikiwa ufisadi, ukabila na siasa chafu zitazimwa ili kila mtu ajitose katika kazi na kuzidisha ari ya kuboresha uchumi. Hii si jukumu la serikali pekee, linahitaji uwajibikaji kutoka mashrika za kibinafsi na raia kwa ujumla.
Na ndiposa safu hiii inapiga darubini kuhusu kibarua cha atakayemrithi rais Uhuru Kenyatta baada ya uchaguzi . Taifa hili haliitaji wenye porojo ambao kamwe hamna matendo. Kenya inahitaji Thomas Sankara, Sere Sekama na Hayati rais wa Tanzania, Pombe Magufuli ili kunyorosha na kurudisha nidhamu serikalini.
Sera zao ziwe za kuleta mtazamo mpya katika jamii ya mkenya na inayolenga kuweka taifa hili miongoni mwa mataifa yenye ruwaza ya Afrika 2063. Tusiruhusu siasa na mikwaruzano kusambaratisha jamii yetu kama vile nchi za Nigeria, Rwanda, na Congo ambazo zingine hadi wa leo zinashuhudia michafuko