- Viongozi wa Azimio, Kenya Kwanza wazuru Bomas huku kura zikiendelea kuhesabiwa
Vinara wa Azimio la Umoja One Kenya na wenzao wa Kenya Kwanza Jumatano usiku walizuru Bomas of Kenya ambapo uwasilishaji wa mwisho wa matokeo ya urais ulikuwa ukiendelea.
Bomas of Kenya ndio kituo kikuu cha kitaifa cha kujumlisha kura katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Viongozi kutoka timu ya Azimio waliozuru kituo hicho ni pamoja na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed na Gavana wa Mombasa Hassan Joho.
Gavana wa Kitui Charity Ngilu pia alikuwepo.
Wenzao wa Kenya Kwanza waliopo kituoni ni pamoja na maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho) na aliyekuwa mbunge mteule Wilson Sossion.
Wengine ni Wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Gladys Shollei (Mbunge wa Uasin Gishu) na Gavana wa Nandi Stephen Sang miongoni mwa wengine.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anatarajiwa kutoa mkutano wake wa tatu na wanahabari tangu kuanza kwa shughuli ya kujumlisha kura.