Wakili Awadhihaki Wapiga Kura Kwa Kutomchagua "Akili Zao na Zangu Hazikutani"

"Upeo wa kiakili kati ya wapiga kura na mimi mwenyewe ulikuwa mpana sana kuwezesha mkutano wa akili zetu,”

Muhtasari

• “Usitukane wapiga kura, jaribu tena kipindi kingine na usiongee kizungu ukienda huko,” mmoja kwa jina Oscar Goodman alimshauri.

Wakili Levis Munyeri aliyekuwa akigombea ubunge Mukurweini
Wakili Levis Munyeri aliyekuwa akigombea ubunge Mukurweini
Image: Levis Munyeri//Facebook

Wakili mmoja kwa jina Levi Munyeri amegonga vichwa vya habari baada ya kuonekana kuwarushia tope wananchi kwa kile alidokeza kwamba walikosa kumpigia kura kwa sababu jinsi ya kufikiria kwake na kwqa wananchi kulikuwa hakutangamani.

Munyeri ambaye alikuwa anawania ubunge Mukurweini kwa tikiti ya chama cha Republican Liberty Party alidokeza kukubali kushindwa uchaguzi huo licha ya matokeo rasmi kutolewa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.

Kukubali kwake kushindwa hata hivyo hakukuja kwa njia rahisi kama ambavyo tumewaona wengi wakikubali na kuwahongera washindi bali yeye alionekana kumenyana na wakaazi wa Mukurweini kwa maneno huku akiwadhihaki kwamba hawangeweza kufikiria sawa na yeye na ndio maana walimuangusha.

“Ninakubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha ubunge wa Mukurwe-ini. Upeo wa kiakili kati ya wapiga kura na mimi mwenyewe ulikuwa mpana sana kuwezesha mkutano wa akili zetu,” Levis Munyeri alikubali matokeo kwa kudhihaki wapiga kura wa eneo bunge hilo.

I concede defeat in the Mukurwe-ini parliamentary race. The intellectual margin between the electorate and myself was too wide to enable the meeting of minds.

Posted by Levi Munyeri on Wednesday, August 10, 2022

Wananchi walitolea maoni kinzani kuhusu maneno haya ambayo wakili Munyeri aliandika na wengine walichukua fursa hiyo kumshauri jinsi ya kukubali matokeo na pengine kufikiria kujaribu baadae tena.

“Usitukane wapiga kura, jaribu tena kipindi kingine na usiongee kizungu ukienda huko,” mmoja kwa jina Oscar Goodman aliandika.

“Kauli yako inaweza isiende vizuri kwa watu wengi. Unaweza kumaanisha vizuri lakini cha muhimu ni jinsi watu wanavyotafsiri hili,” mwingine kwa jina Mugambi Mutua alimshauri.

Wakili huyu anajiunga na orodha ambayo inazidi kunenepa ya wanasiasa ambao wanajitokeza wazi kukubali matokeo baada ya kushindwa na kuwapongeza washindani wao.

Awali, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alikubali kushindwa ugavana wa Kiambu huku pia mbunge wa Lang’ata Generali Nixon Korir naye akidokeza kukubali kushindwa na kumpongeza mshindani wake mtangazaji Phelix Odiwuor.

Pia mbunge wa Embakasi Magharibi George Theuri alikubali matokeo na kumpa shavu mshindani wake Muriithi Mwenje kutoka chama cha Jubilee.