Baadhi ya Majina Makubwa Katika Sanaa Yaliyodunishwa Kwenye Siasa

Inasemekana kuwa katika siasa, siku ni muda mrefu sana.

Muhtasari

• Mtangazaji maarufu wa redio na emcee Mary Njambi Koikai alikuwa ameelekeza macho yake kwenye kiti cha ubunge cha Dagoretti Kusini.

 

Mchekeshaji na mwanasiasa Jasper Muthomi almaarufu MC Jessy
Mchekeshaji na mwanasiasa Jasper Muthomi almaarufu MC Jessy
Image: INSTAGRAM//MC JESSY

Kenya inapoingia siku ya pili ya kuhesabu na kujumlisha kura, majina maarufu na mashuhuri pia yamejitokeza sana katika orodha ya washindi na walioshindwa.

Majina makubwa katika tasnia ya burudani ambao walikuwa wamechagua kujaribu karata chafu ya siasa hawajaachwa nyuma, wengine wakipata matokeo chanya, huku wengine wakipata uzoefu ambao labda hawakuwa tayari wa kubwagwa bila huruma.

Wengi wao watachagua funzo ambalo watalazimika kuishi nalo maisha yao yote. Inasemekana kuwa katika siasa, siku ni muda mrefu sana. Hii hapa orodha ya baadhi ya watu mashuhuri ambao wameshinda na wengine waliokubali kushindwa hata kabla ya IEBC kutangaza matokeo.

 

Mwanahabari Davidson Ngibuini, maarufu kama DNG, ameshinda kiti cha Woodley, Kenyatta Golf Course Wadi. Akiwania chini ya chama cha UDA cha Naibu Rais William Ruto, alimshinda MCA Mwangi Njihia wa Jubilee Party.

Bado Woodley, mmoja wa wanachama wa kundi la P-unit, Gabriel Kagundu, maarufu kama Gabu, alikuwa akitafuta nafasi hiyo hiyo na Alliance National Congress (ANC).

Alikubali kushindwa baada ya DNG kushinda kiti hicho. Msanii wa Kenya Kevin Kioko almaarufu Bahati, ambaye alikuwa akiwania kwa tikiti ya Jubilee Party, alipoteza azma yake ya kuwa mbunge wa Mathare. Alikuwa akitafuta kurithi nafasi ya Anthony Oluoch ambaye amesemekana huenda akakitetea kiti hicho.

Wengine ambao pia walibwagwa na kukubali matokeo ni pamoja na aliyekuwa mtangazaji Boniface Musambi aliyekuwa akiwania ubunge Kitui ya kati na pia mchekeshaji Jasper Muthomi almaarufu Jessy MC aliyetupwa nje katika eneo bunge la South Imenti.

Mtangazaji maarufu wa redio na emcee Mary Njambi Koikai alikuwa ameelekeza macho yake kwenye kiti cha ubunge cha Dagoretti Kusini.

"Napenda kumpongeza mshindi (ambaye bado hajatangazwa) kwa kuchaguliwa kwao na ninawatakia kila la kheri katika kuendeleza matumaini ya wapiga kura wetu," alisema hata kabla ya matokeo rasmi kutolewa.

Mchekeshaji John Kiarie safari hii hakuwa na bahati kwani baada ya kuhudumu bungeni kwa muhula mmoja kama mbunge wa Dagoretti Kusini, alibwagwa nje na mbunge wa zamani Dennis Waweru.