Chris Wamalwa akubali kushindwa na Natembeya katika kinyang'anyiro cha ugavana Trans Nzoia

Mbunge huyo anayeondoka pia alimpongeza Natembeya kwa kutwaa ushindi.

Muhtasari

•Wamalwa pia alimpongeza mgombeaji wa DAP-K George Natembeya akisema ameshinda kinyang'anyiro hicho.

Mbunge Chris Wamalwa.
Image: MAKTABA

Mgombea ugavana wa Trans Nzoia kwa tiketi ya Ford Kenya Chris Wamalwa amekubali kushindwa.

Katika taarifa aliyochapisha Twitter, Wamalwa aliwashukuru wapiga kura wa Trans Nzoia na chama chake kwa uungwaji mkono waliompa katika kipindi chote cha kampeni.

Mbunge huyo wa zamani wa Kiminini pia alimpongeza mgombeaji wa DAP-K George Natembeya akisema ameshinda kinyang'anyiro hicho.

"Namtakia heri," Wamalwa alisema.

"Sijafaulu katika azma yangu ya kuwa Gavana wa pili wa Kaunti yetu kuu. Namshukuru Mwenyezi Mungu, wafuasi wangu wote kutoka mbali na karibu, kwa usaidizi wao usio na kikomo. Pokeeni shukrani zangu za milele," aliongeza.

Mbunge huyo anayeondoka pia aliwashukuru wananchi wa jimbo la Kiminini kwa kumchagua kuwa mbunge kwa vipindi viwili mfululizo.

"Shukrani zangu za dhati kwa wafuasi wa chama na watu wa kujitolea ambao wamefanya kazi kubwa katika kampeni hii," alisema.