Matokeo ya muda yanadokeza kuwa mchuano mkali wa urais nchini Kenya kati ya Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani.
Kwa zaidi ya 90% ya matokeo yaliyotumwa kutoka kwa maelfu ya vituo vya kupigia kura, hesabu za ndani zinaonyesha pengodogo sana kati ya wagombeaji hao wawili .
Lakini kwanini kuna matokeo tofauti katika kumbi mbali nchini Kenya ?
Kwanza ,unafaa kujua kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka imeziweka fomu za matokeo hayo za 34A na 34B katika tovuti yake.Vyombo vya habari,vyama vya kisiasa na hata raia wanaweza kuzichukua fomu hizo na kuanza kujumlisha hesabu hizo.
Hiyo ndio sababu kubwa ya matokeo tofauti kwa sababu hakuna mpangalio maalum au wa kufanana wa kuzichukua fomu hizo na kila anayefanya hesabu hizo anaanza na idadi fulani ya fomu ambazo anaweza kuzijumlisha na kisha kutoa matokeo ya muda.Wanaofanya hivyo wapo katika awamu tofauti ya zoezi la kuzijumlisha hivyo basi kusababisha tofauti ya matokeo ambayo yanaonekana .
Hata hivyo inaweza kuchukua siku kadhaa kabla ya matokeo rasmi kujulikana.
Kura hiyo ya Jumanne ilifuatia kampeni iliyotawaliwa na mijadala kuhusu gharama za maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.
Waliojitokeza kupiga kura wanakadiriwa kuwa karibu 64%, pungufu ya 80% katika uchaguzi uliopita miaka mitano iliyopita.
Hata hivyo, mkuu wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati amesema idadi hii itaongezeka pindi data itakapopatikana kuhusu wapiga kura ambao walithibitishwa kwa sajili ya daftari badala ya kupitia kitambulisho cha kielektroniki (KIEMS).