"Umenionyesha ukomavu, sitasahau kamwe!" Jalang'o ampongeza Korir kwa kukubali kushindwa

"Mwanaume gani! Asante Nixon Korir. Umenionyesha ukomavu ni nini! Sitasahau kamwe! Asante," Jalas alisema.

Muhtasari

•Jalang'o alitangazwa mshindi  baada ya kujizolea  kura 38, 948 dhidi ya  36,836 za Korir ambaye alichukua nafasi ya pili.

•Jalang'o alimshukuru Korir kwa kukubali kushindwa na kumpongeza hata kabla ya matokeo ya kura kutangazwa.

Nixon Korir na Jalang'o
Image: INSTAGRAM// JALANG'O

Mbunge mteule wa Lang'ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang'o ameridhishwa na jinsi mpinzani wake mkuu Nixon Korir alivyojiendesha baada ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika mapema wiki hii.

Jalang'o ambaye aliwania ubunge wa eneo hilo kwa tiketi ya ODM alitangazwa mshindi  baada ya kujizolea  kura 38, 948 dhidi ya  36,836 za Korir ambaye alichukua nafasi ya pili.

"Asante Langata kwa kunipa nafasi ya kuwatumikia  kama mbunge wenu! Nina mengi ya kusema lakini kwa sasa naomba mkubali Asante yangu! Huu sio ushindi wangu! Ni ushindi wenu watu wa Langata!! Wacha tutembee safari hii pamoja!," Jalang'o alisema baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi.

Huku akiwahutubia wakazi baada ya kukabidhiwa cheti, mtangazaji huyo wa zamani aliwaomba washindani wake wote kukubali kufanya kazi pamoja naye wakati anapochukua uwakilishi wa eneo bunge hilo la kaunti ya Nairobi. 

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Korir kwa kukubali kushindwa na kumpongeza hata kabla ya matokeo ya kura kutangazwa.

"Tunatoa shukrani zetu kwa mshindani wetu ambaye tayari alikuwa amekubali kushindwa. Lakini tunataka kufanya kazi pamoja. Ushindi huu sio wangu. Ni kwa ajili ya watu wa Lang'ata. Tukuje pamoja sote kwa ajili ya watu wa Lang'ata. Kila mtu tuliokuwa tukishindana naye ninawakaribisha ili tuweze kujenga Lang'ata tena," Alisema.

Korir ambaye amewakilisha eneo hilo tangu mwaka wa 2017 alikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia Jalang'o akikabidhiwa cheti cha ushindi.

Mgombea huyo wa UDA alimpa Jalang'o salamu za ushindi na hata kuhutubia umati, hatua ambayo mbunge huyo mteule amepongeza.

"Mwanaume gani! Asante Nixon Korir. Umenionyesha ukomavu ni nini! Sitasahau kamwe! Asante," Jalas alisema.

Jumatano Korir alikubali kushindwa na mchekeshaji huo na kuwashukuru wakaazi wa Lang’ata kwa kumpa nafasi ya kuwahudumia bungeni.

"Kwa wananchi wa Langata, ninawashukuru kwa dhati kwa kunipa nafasi ya kuwa Mbunge wenu kwa miaka 5 iliyopita. Imekuwa ni fursa nzuri ambayo ilinipa nafasi ya kuchangia ujenzi wa taifa letu na huduma kwa watu. Kutokana na matokeo ambayo tumejumlisha katika kituo cha Generali, mshindani wangu Jalango anaongoza na ninataka kumpongeza anapojiandaa kutwaa taji hilo na kuisogeza mbele Langata. Siasa si chuki. Mungu ambariki Langata,”Korir alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.