Wa Jungle ataka za ugavana kura za ugavana Kiambu kuhesabiwa upya

Wa Jungle alisema mchakato wa kuhesabu kura ulikuwa duni na ulikumbwa na dosari.

Muhtasari

•Mgombea huru wa ugavana wa Kiambu Patrick Wainaina 'Wa Jungle' sasa anataka kura zihesabiwe upya.

•Wa Jungle alishutumu maafisa wasimamizi wa uchaguzi wa Kiambu kwa kufanikisha makosa.

Wainaina Wa Jungle na mgombea mwenza Ann Nyokabi wakihutubia wanahabari Agosti 11,2022
Wainaina Wa Jungle na mgombea mwenza Ann Nyokabi wakihutubia wanahabari Agosti 11,2022
Image: AMOS NJAU

Mgombea huru wa ugavana wa Kiambu Patrick Wainaina 'Wa Jungle' sasa anataka kura zihesabiwe upya.

Akihutubia wanahabari Alhamisi, Wa Jungle alisema mchakato wa kuhesabu kura ulikuwa duni na ulikumbwa na dosari.

"Tunataka kuhesabiwa upya kwa kura kwa kuwa mchakato haujakuwa huru na wa haki," Wa Jungle alisema.

Alishutumu maafisa wasimamizi wa Kiambu kwa kufanikisha makosa.

“Hatutaruhusu hitilafu hizo kutokea na wananchi wa Kiambu lazima waruhusiwe kuwachagua viongozi wao kwa busara,” akasema.

Wajungle alisema ataelekea mahakamani ikiwa IEBC haitaamuru kuhesabiwa upya.

Naibu wake Ann Nyokabi alisema kuwa hawataacha chochote.

Hapo awali, aliyekuwa mbunge mteule Isaac Mwaura alikuwa amemkashifu msimamizi wa uchaguzi Beatrice Muli kwa kuwa na kiburi.

Mwaura alisema takriban kura 1,394 zilizoegemea upande wa naibu rais hazikuwepo.

“Baada ya kuibua suala hilo, kura za Ruto ambazo hazikuwepo zimeongezwa na tunashukuru sana,” Mwaura alisema.

Afisa wa uchaguzi katika kaunti ya Kiambu Beatrice Muli alithibitisha tofauti hiyo na kuitaja kama hitilafu ya uchapishaji.

Alisema kuwa maajenti wote walikubali na tatizo likatatuliwa.

"Ni kweli, kura 1394 kutoka mikondo minne hazikuwepo na tumerekebisha," alisema.