Zifahamu kaunti ambazo tayari zimemaliza kuwasilisha matokeo ya urais

Jumla ya vituo 46,014 kati ya 46,229 tayari vimefanikiwa kutuma fomu 34A.

Muhtasari

•Kaunti hizo ni pamoja na Nyeri, Siaya, Tharaka- Nithi, Uasin Gishu, Vihiga, Kirinyaga, Makueni, Mombasa na Murang'a.

•Jumla ya vituo 46,014 kati ya 46,229 vilikuwa vimefanikiwa kutuma fomu 34A wakati wa kuwasilisha ripoti hii.

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 10, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 10, 2022
Image: ENOS TECHE

Radio Jambo sasa inaweza kufichua idadi ya kaunti ambazo tayari zimesambaza fomu 34A kutoka vituo vyao vya kupigia kura hadi vituo vya kujumlisha kura vya eneo bunge.

Katika kituo cha kujumlisha kura cha eneo bunge, fomu 34A hupewa msimamizi wa eneo bunge, ambaye hujaza fomu 34B kabla ya kuikabidhi kwa msimamizi wa uchaguzi wa urais.

Kaunti hizo ni pamoja na Nyeri, Siaya, Tharaka- Nithi, Uasin Gishu, Vihiga, Kirinyaga, Makueni, Mombasa na Murang'a.

Nyingine ni Nyamira, Nyandarua, Kilifi, Kericho, Homabya, Embu, Elegeyo Marakwet, Diaspora, Bungoma na Bomet.

Nyeri, Bomet, Elgeyo Marakwet, Kericho na Uasin Gishu zilikuwa miongoni mwa kaunti za kwanza kuwasilisha fomu zao.

Kumekuwa na changamoto kadhaa zilizoripotiwa na ucheleweshaji katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, jambo ambalo linaeleza kwa nini baadhi yao bado hawajawasilisha nusu ya matokeo.

Kufikia Agosti 11, mwendo wa saa sita na dakika tano usiku, karibu kaunti zote zilikuwa zimewasilisha angalau asilimia 99.37 ya matokeo. Hata hivyo, kaunti ya Wajir ilikuwa imewasilisha asilimia 81.31 pekee.

Jumla ya vituo 46,014 kati ya 46,229 vilikuwa vimefanikiwa kutuma fomu 34A wakati wa kuwasilisha ripoti hii.

Shirika la uchaguzi linatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya kura ya urais ndani ya siku saba kutoka siku ya kupiga kura.

"Matokeo katika tovuti ya umma ni yale yale ambayo tume itatumia kutangaza matokeo," mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema.

"Ukusanyaji wa matokeo kutoka maeneobunge 290 unaendelea na wasimamizi wa uchaguzi watatoa Fomu 34B baadaye."