Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amefanikiwa kutetea kiti chake kwa tikiti ya UDA dhidi ya mshindani wake wa karibu aliyekuwa mwakilishi wa wanawake, Purity Wangui Ngirici.
Waiguru alijizolea kura 113,088.
"Kutokana na hayo matokeo yaliyotangulia, namtangaza Anne Mumbi Waiguru kuwa Gavana mteule wa Kaunti ya Kirinyaga," Msimamizi wa Uchaguzi wa Kaunti alitangaza.
Ngirici ambaye aligombea kama mgombeaji binafsi alikuwa na kura 105,677.
Awali kulikuwepo na fujo katika kituo cha kuhesabu kura eneo bunge la Gichugu ambapo Ngirici aliibua madai ya kutaka uhesabu wa kura kurudiwa katika eneo hilo baada ya kusema kwamba hakuridhika na jinsi hesabu ya awali ilivyofanywa. Baada ya vuta nikuvute ya muda hatimaye msimamizi wa kituo hicho alikubali kurudia kuhesabu kura hizo na kupata matokeo sawia na ya awali.
Aidha mapema juzi kuliibuka na uvumi wa uongo ulioenezwa kwamab Ngirici ameshinda mpaka mgombea mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Martha Karua akapeleka kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kumpongeza kwa kumshinda Waiguru ambaye ni hasimu wake wasiyeonana jicho kwa jicho ila matokeo rasmi yametangazwa Ijumaa alasiri kudhibitisha kwamba Waiguru anajinyakulia kipindi cha pili na cha mwisho kikatiba kuhudumu kama gavana wa kaunti ya Kirinyaga.
Waiguru alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa gavana 2017 kwa tiketi ya chama cha Jubilee. Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amefanikiwa kutetea kiti chake.
Kaunti ya Kirinyaga licha ya kuwa nyumbani kwa Martha Karua wa Azimio ilionekana kuegemea upande wa Kenya Kwanza huku chama cha UDA chake William Ruto kikinyakua viti vingi huko licha ya Karua na katibu wa kudumu katika wizara ya usalama, Karanja Kibicho kumpigia debe Raila Odinga kaunti hiyo.