Wakenya kote nchini walipiga kura zao kwa viti mbalimbali vya uchaguzi Jumanne, Agosti 9.
Upigaji kura ulimalizika kwa amani na kufikia wakati wa kuchapishwa, matokeo ya Wabunge wa Bunge la Kitaifa na yale ya bunge la kaunti yalikuwa yametangazwa.
Kati ya Kaunti 47, ni Kaunti 45 pekee zilizoshiriki uchaguzi wa viti vyote sita vya kuchaguliwa.
Kaunti za Mombasa na Kakamega, hata hivyo, hazikushiriki uchaguzi wa ugavana.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisitisha zoezi hilo baada ya mkanganyiko wa uchapishaji wa karatasi za kura.
Alisema karatasi za kupigia kura za maeneo hayo zilikuwa na picha na maelezo yasiyo sahihi ya wagombea.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji kura Jumanne, utangazaji wa matokeo ya viti vya ugavana ulianza Alhamisi, Agosti 11.
Haya hapa ni baadhi ya matokeo yaliyopokelewa na Radio Jambo.
Kaunti ya West Pokot
Mgombea wa chama cha UDA Simon Kachapin alishinda baada ya kujizolea kura 86,476. Gavana aliye madarakani John Lonyangapuo aliibuka wa pili kwa kura zaidi ya 84,610.
Kaunti ya Nandi
Stephen Sang amehifadhi kiti chake baada ya kupata kura 237,045.
Mgombea huyo wa UDA alimshinda mpinzani wake aliyekuwa Gavana Cleophas Lagat aliyepata kura 54,375.
Kaunti ya Busia
Chama cha ODM kilidumisha kiti hicho kupitia Paul Otuoma aliyepata 164,478. Mgombea wa ANC John Sakwa aliingia kwa kura 92,144.
Kaunti ya Migori
Ochilo Ayacko wa ODM alishinda kiti hicho kwa kura 175,226. Mpinzani wake wa DAP-K John Pesa alifuata mkia kwa kura 126,171.
Kaunti ya Meru
Kawira Mwangaza kwa tiketi ya kujitegemea ameshinda kiti hicho.Amemshinda aliyemaliza muda wake Kirauti Murungi.
Kaunti ya Vihiga
Wilber Ottichilo wa Chama cha ODM ametetea kiti chake kwa kura 82,313.
Aliyekuwa gavana Moses Akaranga aliibuka wa pili kwa kura 42,432
Kaunti ya Homa Bay
Gladys Wanga wa ODM alishinda baada ya kupata kura 244,559. Evans Kidero aliibuka wa pili kwa kura 154,182.
Kaunti ya Kisumu
Anyang’ Nyong’o wa ODM ameshinda kiti chake baada ya kupata kura 319,957.
Wa pili katika kinyang’anyiro hicho alikuwa Jack Ranguma wa NDG aliyepata kura 100,600.
Kaunti ya Uasin Gishu
Jonathan Chelilim Bii maarufu Koti Moja amenyakua kiti hicho kwa kura 214,036.
Mgombea huru Zedekia Bundotich aliibuka wa pili kwa kura 127,013.
Kaunti ya Bomet
Hilary Barchok amechaguliwa tena kuwa Gavana baada ya kushinda kwa kura 158,798 akimshinda mpinzani wake mkuu Isaac Rutto aliyepata kura 137,323.
Trans Nzoia
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, George Natembeya ameshinda baada ya kupata kura 158,919.Mshindani wake Chris Wamalwa wa Ford Kenya aliibuka wa pili kwa kura 79,020.
Kaunti ya Isiolo
Abdi Hassan Guyo wa chama cha Jubilee ameshinda kiti hicho baada ya kupata kura 28,664.Alimshinda mpinzani wake mkuu Godana Doyo aliyepata kura 2,551 chini ya tikiti ya Independent.
Kaunti ya Siaya
Seneta wa ODM James Orengo ameshinda kiti hicho kwa kura 220,349 akimshinda mshindani wake Nicholas Gumbo aliyeibuka wa pili kwa kura 147,558.
Kaunti ya Nyamira
Mgombea wa chama cha United Progressive Alliance Amos Nyaribo amechaguliwa tena kuwa Gavana wa Kaunti ya Nyamira baada ya kupata kura 82,090.Mpinzani wake wa karibu Walter Nyambati wa UDA alipata kura 49,281.
Kaunti ya Isiolo
Abdi Hassan Guyo ameshinda kiti hicho chini ya tikiti ya chama cha Jubilee baada ya kupata kura 28,664. Alimshinda mpinzani wake mkuu Godana Doyo aliyepata kura 2,551 chini ya tikiti ya Independent.
Kaunti ya Kirinyaga
Ann Waiguru wa UDA amechaguliwa tena baada ya kupata kura 113,088 baada ya kumshinda Wangui Purity aliyekuwa na kura 105,677.
Matokeo zaidi yanafuata...