Naibu Gavana wa Kwale anayeondoka Fatuma Achani sasa ndiye gavana mteule wa kaunti hiyo.
Achani alitangazwa Ijumaa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Kaunti Obadiah Kariuki katika kituo kikuu cha kuhesabia kura cha Kenya School of Government, eneo bunge la Matuga.
Achani alishinda kinyang’anyiro hicho kwa tiketi ya UDA baada ya kuwabwaga profesa Hamadi Boga wa ODM, Chirau Ali Mwakwere wa Wiper, Gereza Dena (KANU), Lung’anzi Chai Mangale (PAA), na Sammy Ruwa (Huru).
Alipata kura 59,674 huku Boga akipata kura 53, 972.
Lung'anzi alishika nafasi ya tatu kwa kura 47,301.
Achani alichuana kwa tikiti ya chama cha UDA baada ya gavana anayeondoka Salim Mvurya kutofautiana na vyama vya ODM na Jubillee katika muhula wao wa kwanza na wa pili.
Katika nafasi ya useneta, Issa Boya wa ODM alidumisha kiti chake kwa kuzoa kura 52, 772.
Alifuatiwa na Antony Yama wa UDA aliyepata kura 41, 762, Salim Mwadumbo wa ANC aliyepata kura 16, 902, na William Ndeti wa DP kura 9,236.
Takriban wagombea tisa walijitokeza kuwania kiti cha useneta.
Fatuma Masito wa ODM alitangazwa kuwa mwakilishi mpya wa wanawake baada ya kupata kura 58,820.
Bibi Masha (UDA) ndiye aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kupata kura 44,472 akifuatiwa na Zainab Chitsangi (Independent) aliyekuwa na kura 35,633.