Malombe akinyakua tena kiti cha ugavana Kitui

Malombe alipata kura 198,004 huku mpinzani wake wa karibu David Musila akiibuka wa pili kwa kura 114,606.

Muhtasari

•Malombe alipata kura 198,004 huku mpinzani wake wa karibu na ambaye ni seneta wa zamani David Musila wa chama cha Jubilee akiibuka wa pili kwa kura 114,606.

•Macharia alimtangaza Malombe kuwa gavana mteule na kumkabidhi cheti dakika chache kabla ya saa tano usiku.

Gavana mteule wa Kitui Julius Malombe (katikati) na naibu wake Augustine Kanani wapokea cheti kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa Kaunti ya Kitui Macharia Gichichi mara baada ya kuwatangaza washindi katika kituo cha Mafunzo cha Kitui Multipurpose Ijumaa usiku.
Gavana mteule wa Kitui Julius Malombe (katikati) na naibu wake Augustine Kanani wapokea cheti kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa Kaunti ya Kitui Macharia Gichichi mara baada ya kuwatangaza washindi katika kituo cha Mafunzo cha Kitui Multipurpose Ijumaa usiku.
Image: MUSEMBI NZENGU

Aliyekuwa gavana wa Kitui Julius Makau Malombe amerejea kutwaa kiti hicho alichopoteza kwa Charity Ngilu mwaka wa 2017.

Malombe alipata kura 198,004 huku mpinzani wake wa karibu na ambaye ni seneta wa zamani David Musila wa chama cha Jubilee akiibuka wa pili kwa kura 114,606.

Jonathan Mueke wa UDA, ambaye ni naibu gavana wa zamani wa Nairobi, alipata kura 10,639.

Matokeo hayo yalitangazwa Ijumaa usiku na afisa wa uchaguzi wa Kaunti ya Kitui Macharia Gichichi katika jumba la Kitui Multipurpose Development and Training Centre ambalo limegeuzwa kuwa kituo cha kujumlisha kura za kaunti ya IEBC.

Ingawa gavana wa Kitui Ngilu alikuwa amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa kuchelewa, jina lake lilikuwa kwenye kura na pia alipata kura 2026.

Macharia alimtangaza Malombe kuwa gavana mteule na kumkabidhi cheti dakika chache kabla ya saa tano usiku.

Umati wa wafuasi wa Malombe waliokuwa wamemsindikiza na kupiga kambi nje ya lango la taasisi hiyo waliimba na kucheza kwa furaha baada ya kutangazwa mshindi.

Malombe aliandamana na naibu wake mteule, Augustine Wambua Kanani, mwakilishi wa Wanawake Irene Kasalu na Seneta wa Kitui Enoch Wambua.

Wambua na Kasalu wote walitangazwa washindi baada ya kuhifadhi viti vyao vya Seneti na uwakilishi wa wanawake mtawalia.

Wambua alipata kura 191,317 huku Kasalu akiambulia kura 201,899 kuhifadhi viti vyao.