Rais Uhuru Kenyatta Jumamosi atakutana na viongozi wote wapya waliochaguliwa wa Azimio kuanzia saa nne asubuhi Jijini Nairobi. Haijabainika ni nini ajenda ya mkutano huo na ikiwa mkutano utakuwa Ikulu au KICC.
Lakini vyanzo vinasema rais anataka kukagua utendakazi wa muungano wake na kukubaliana juu ya njia ya kusonga mbele.
Rais pia anatarajiwa kuzungumzia matokeo ya urais ambayo bado hayajawasilishwa kikamilifu na kutangazwa na IEBC.
Haya yanajiri saa chache baada ya katibu wa mawasiliano wa Raila Odinga, Dennis Onsarigo kusema Azimio la Umoja itaandaa kongamano la uzinduzi wa wanachama wake waliochaguliwa baadaye mchana. Onsarigo alisema mkutano huo utafanyika KICC kuanzia saa 10 asubuhi.
Wahudhuriaji wameombwa kuvalia rangi za buluu za Azimio.
Muungano wa Azimio umeshinda viti 147 vya wabunge, viti saba vya Seneti na viti 10 vya ugavana, kulingana na fomu zilizothibitishwa kufikia sasa.
Siku tatu baada ya uchaguzi kukamilika, asilimia 99 ya matokeo kutoka vituo vya kupigia kura yamewasilishwa kwa njia ya kielektroniki.
Ni idadi ndogo tu ndiyo imethibitishwa na kutangazwa na Tume Huru na ya Mipaka ya Uchaguzi.
Kungoja huko kumeongeza wasiwasi kote nchini huku Wakenya wakisubiri kwa hamu kumpata mshindi wa kinyang’anyiro cha urais.
Matokeo ya muda yalionesha mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na Naibu Naibu William Ruto wakiwa wameshikana kinyang'anyiro hicho.
Kulingana na katiba, IEBC ina hadi Agosti 15 kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais na tayari zimesalia chini ya saa 48 kwa makataa hayo kukamilika huku mchakato wa IEBC kuhakikisha kura na fomu za 34A ukiwa umefika kwa maeneo bunge takribani 50 kati ya maeneo bunge 290 pamoja na lile moja linalowakilisha kura kutoka kwa wakenya wanaoishi nchi za nje.
Kulingana na matokeo hayo yanayoendelea kutiririshwa na IEBC kutoka ukumbi wa Bomas, washindani Raila Odinga wa Azimio na William Ruto wa UDA wanazidi kukabana koo kwa ukaribu mno huku upande wowote ukiwa na matumaini ya kuibuka washindi pindi tu udhibitishwaji wa fomu hizo kutoka maeneo bunge yote utakapokamilika.