"Tutapinga Matokeo ya Uchaguzi" - Viongozi wa Jubilee Kutoka Mt. Kenya

"Hakuna kitu kama wimbi la UDA katika Mlima Kenya kwani mchakato uligubikwa na dosari,"

Muhtasari

• Mgombea ubunge wa Thika Gakuyo alisema kuwa shughuli nzima ilikuwa ya udanganyifu na watawasilisha ombi mahakamani.

Viongozi wa Jubilee wakihutubia wanahabari Agosti 13.
Viongozi wa Jubilee wakihutubia wanahabari Agosti 13.
Image: STAR//AMOS NJAU

Mgombea wa kiti cha ugavana Kiambu James Nyoro amesema kuwa watapinga matokeo ya IEBC ambayo yaliwaangusha wanasiasa wengi katika eneo la mlima Kenya ambao walikuwa wakigombea kutoka vyama chini ya mwavuli wa Azimio ambao walishindwa kwa wingi na wagombea kutoka UDA.

Akihutubia wanahabari, Nyoro aliwataka Wakenya kusalia na amani huku wakipanga kuwasilisha malalamishi yao baada ya kukamilika kwa mchakato wa kujumlisha kura.

Aliandamana na George Mara (mgombea Useneta), David Gakuyo (Thika Town), Owen Ndungu (Kikuyu), Damaris Wambui ( Kiambaa) na naibu wake June Waweru.

Mgombea kiti cha useneta wa Jubilee George Mara alisema kuwa watamaliza chaguzi zote zinazopatikana.

"Hatutakubali matokeo au kuwapongeza wapinzani wetu bado," alisema.

Mwakilishi wa wanawake kwa tiketi ya Jubilee Gladys Chania alisema kuwa kulikuwa na dosari nyingi, haswa katika eneo la mlima Kenya ambako UDA ilionesha vyama vingine kama Jubilee vumbi ya karne.

Mgombea ubunge wa Thika Gakuyo alisema kuwa shughuli nzima ilikuwa ya udanganyifu na watawasilisha ombi mahakamani.

"Hakuna kitu kama wimbi la UDA katika Mlima Kenya kwani mchakato uligubikwa na dosari," alisema.

Mgombea wa Jubilee Kiambaa Damaris Waiganjo alisema kuwa maajenti wake hawakuruhusiwa na alilazimika kuingilia kati.

"Tunajua kilichotokea na IEBC inafaa kuamuru kuhesabiwa upya kwa kura," alisema.

Malalamishi haya yanatokea siku chache tu baada ya kukamilika kwa kupiga kura ambapo baadhi ya wagombea wa Jubilee walioshindwa walikiri hadharani na kuwapongeza washindani wao ambao walikuwa kutoka chama cha WilliamRuto, UDA.

Kanini Kega wa Kieni, Jeremiah Kioni wa Ndaragua na Amos Kimunya wa Kipipiri ni baadhi ya wabunge wanaoondoka wa Jubilee waliokubali matokeo baada ya kubwagwa.

Viongozi wa Jubilee wakihutubia wanahabari Agosti 13.
Viongozi wa Jubilee wakihutubia wanahabari Agosti 13.
Image: STAR//AMOS NJAU