Igathe akubali matokeo na kumhongera Sakaja kwa ushindi

Sakaja alitangazwa kuwa mshindi kwa kura 699, 392

Muhtasari

• Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Nairobi, Albert Gogo alimtangaza Sakaja aliyekuwa akiwania kwa chama cha UDA kuwa mshindi

Aliyekuwa mgombea wa ugavana Nairobi, Polycarp Igathe
Aliyekuwa mgombea wa ugavana Nairobi, Polycarp Igathe
Image: Facebook//Polycarp Igathe

Aliyekuwa mgombea ugavana Nairobi Polycarp Igathe amenywea na kukubali matokeo ya uchaguzi baada ya mshindani wake Johnson Sakaja kutangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho na kuwa rais wa kaunti hiyo ambayo ni kitovu cha uchumi wa taifa la Kenya.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Igathe amempongeza Sakaja kwa ushindi huo mkubwa na kumtakia kila la kheri katika safari yake ya kuwatumikia wana Nairobi.

“Ninakubali uamuzi wa watu wa Nairobi na kuwashukuru wafuasi wetu wote. Gavana wa Nairobi ni Mheshimiwa Johnson Sakaja. Hongera! Mungu ibariki Kenya,” Polycarp Igathe aliandika.

Msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Nairobi, Albert Gogo alimtangaza Sakaja aliyekuwa akiwania kwa chama cha UDA kuwa mshindi baada ya kupata kura zaidi ya laki sita huku Igathe akiibuka wa pili kwa kura zaidi ya laki tano.

Igathe sasa anajiunga katika orodha ya wanasiasa wengi ambao wamekubali matokeo bila ya kutaka kuyapinga mahakamani kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa katika chaguzi za awali.

Sakaja alimshinda kwa zaidi ya kura laki moja na hili linatajwa kuwa pigo kubwa kwa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya waliokuwa wakitaka kuwa na udhibiti wa jiji la Nairobi katika nyadhifa za juu zote ila Sakaja akavuruga mipango yao.

Igathe sasa anajiunga na Moses Kuria aliyekuwa akiwania ugavana Kiambu kukubali matokeo katika nyadhifa hiyo ya juu katika serikali za ugatuzi.