Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip abwagwa na Joseph Githuku

Alihudumu kama mwakilishi wadi maalum aliyeteuliwa kati ya 2013 na 2017 chini ya Farmers Party.

Muhtasari

• Githuku wa Jubilee Party alimshinda Loitiptip na wagombeaji wengine saba baada ya kupata kura 12,091  kujinyakulia wadhifa huo.

Seneta mteule wa Lamu Joseph Githuku wa Jubilee Party. Picha: PRAXIDES ZANGU
Seneta mteule wa Lamu Joseph Githuku wa Jubilee Party. Picha: PRAXIDES ZANGU

Utawala wenye misukosuko wa Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip umefikia kikomo kufuatia kuchaguliwa kwa Joseph Githuku kama seneta mteule wa Lamu.

Githuku wa Jubilee Party alimshinda Loitiptip na wagombeaji wengine saba baada ya kupata kura 12,091  kujinyakulia wadhifa huo.

Alihudumu kama mwakilishi wadi maalum aliyeteuliwa kati ya 2013 na 2017 chini ya Farmers Party.

Katika kinyang’anyiro hicho, Githuku alifuatwa kwa karibu na wakili maarufu Yusuf Mahmoud Aboubakar aliyepata kura 11,875. Loitiptip alimaliza wa sita kwa kura 2,238.

Ahmed Bunu Haji, ambaye kitaaluma ni daktari, aliwania kwa tikiti ya chama cha ODM na kumaliza wa tatu kwa kura 8,688.

Francis Kariuki Mugo wa UDA alikuwa wa nne kwa kura 7,351.

Wengine katika kinyang’anyiro hicho ni Abdi Omar Mohamed, aliyepata kura 3,179, Abdiwely Mohamed Dhahir wa NAPK aliyepata kura 1,925, Ahmed Suleiman Ali wa Chama cha UPIA akipata kura 1,436 na Khamis Nassor Mbaruk almaarufu Bwangao kura 611.

Kwenye hotuba yake punde tu baada ya kutangazwa mshindi, Githuku aliwashukuru wapiga kura wa Lamu kwa kumchagua na kuahidi kuwa seneta bora na kujitahidi kuafiki maendeleo yanayohitajika katika kaunti hiyo.

Alisema lengo lake kuu litakuwa kuhakikisha mgao wa Lamu unaongezwa kwa maendeleo bora na kuhakikisha maslahi ya wakazi yanawakilishwa kikamilifu katika Seneti.

“Nitawaunganisha wananchi na uongozi wa Lamu ili tuwe na ajenda moja ya Lamu. Pia nitatekeleza jukumu langu la uangalizi kama seneta wa kaunti hii kikamilifu kwa kuhakikisha pesa zinazotengewa Lamu zinatumika vyema,” Githuku alisema.

Aliahidi kushirikiana bega kwa bega na viongozi wengine waliochaguliwa katika kaunti hiyo kuanzia MCAs, wabunge na mwakilishi wa kike na gavana mteule Issa Abdallah Timamy ili maendeleo yapatikane kwa urahisi.

"Viongozi wetu wa awali walishindwa kuleta umoja katika malengo yao. Nitaunga mkono kikamilifu na kufanya kazi pamoja na viongozi wengine wa kaunti ili kutuwezesha kupata maendeleo mahali hapa,” akasema.

Githuku aliahidi kubuni nafasi za kazi kwa vijana, huku pia akiwahakikishia wakazi kuwa matakwa yao watawakilishwa ipasavyo katika Seneti.

“Nina uzoefu katika uongozi, baada ya kuhudumu kama MCA huko Lamu. Kwa hivyo, nitashiriki kikamilifu katika kutunga sheria kwa kuzingatia, kujadili, na kuidhinisha miswada inayohusu Lamu. Sitawaangusha,” alisema.