logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sherehe zatikisa Eldoret na nyumbani kwa Ruto Sugoi baada ya kutangazwa rais

Wakazi wengi wa Eldoret walisema watasherehekea kwa siku kadhaa na kumshukuru Mungu kwa ushindi huo.

image
na

Yanayojiri15 August 2022 - 15:23

Muhtasari


•Sherehe zilisimamisha shughuli katika eneo la Eldoret huku maelfu ya wafuasi wa Ruto wakijitokeza katika barabara za  kusherehekea ushindi.

•Wakazi wengi wa Eldoret walisema watasherehekea kwa siku kadhaa na kumshukuru Mungu kwa ushindi huo.

Sherehe zatikisa mji wa Eldoret baada ya Ruto kutangazwa mshindi mnamo Agosti 15, 2022.

Sherehe zilitanda kote mji wa Eldoret na kijiji cha DP William Ruto cha Sugoi baada ya kutangazwa kuwa rais mteule na IEBC.

Sherehe hizo zilisimamisha shughuli katika eneo hilo huku maelfu ya wafuasi wake wakijitokeza katika barabara za Eldoret kuimba nyimbo na kunengua viuno kusherehekea ushindi wa Ruto.

Wakaazi hao walikuwa wamekesha siku nzima wakitazama shughuli za Bomas of Kenya kwenye runinga kubwa kando ya barabara ya Uganda huko Eldoret.

Barabara hiyo ilikuwa imefungwa siku nzima huku wakazi wengi wakisubiri matokeo ya urais kutangazwa.

"Hii ni moja ya siku bora zaidi maishani mwangu kwa sababu jinsi inavyosemwa ninahisi uhuru umefika", mkazi mmoja Jane Kiptoo alisema.

Wakazi wengi wa Sugoi walionekana wakikimbia hadi nyumbani kwa rais mteule ambayo iko takriban kilomita 30 kutoka Eldoret kutoka kwa barabara kuu kuelekea Webuye.

Usalama uliimarishwa haraka nyumbani ambapo wafanyakazi na wageni walijumuika katika sherehe hizo.

Wakazi walisema walikuwa na furaha tele kwamba mtoto wao amechaguliwa kuwa rais licha ya changamoto nyingi alizopitia katika siasa.

"Ametatizika kutoka kwa mtu wa kawaida na tunamshukuru Mungu kwamba hatimaye amefanikiwa kufika kileleni", alisema mkazi mwingine Paul Kipyego.

Wakazi wengi wa Eldoret walisema watasherehekea kwa siku kadhaa na kumshukuru Mungu kwa ushindi huo.

Mjini Eldoret wakaazi walipeperusha matawi na rangi za kampeni za UDA kuhitimisha sherehe hizo.

Baadhi ya wakazi hata hivyo wamelaani machafuko yaliyoshuhudiwa Bomas wakati wa kutangazwa kwa matokeo.

Sherehe kama hizo pia zilitikisa miji mikuu katika eneo hilo ikijumuisha Kapsabet, Iten, Kapsowar na Kabarnet miongoni mwa mingineyo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved