Uthibitishaji wa fomu wakamilika huku matokeo ya urais yakitarajiwa leo

Ndani ya Bomas, Viti vya Azimio na Kenya Kwanza vilikuwa vimekaliwa kufikia saa tatu asubuhi.

Muhtasari

•Uhakiki wa fomu hatimaye umekamilika Jumatatu asubuhi huku Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikitarajiwa kutangaza matokeo.

•Mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio iko ukumbini zikingoja tangazo kubwa la mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Meza zilizokuwa na mamlaka kamili zilizotumiwa na maafisa kujumlisha na kuthibitisha matokeo zilionekana tupu zikiashiria kumalizika kwa zoezi hilo katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura, Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Meza zilizokuwa na mamlaka kamili zilizotumiwa na maafisa kujumlisha na kuthibitisha matokeo zilionekana tupu zikiashiria kumalizika kwa zoezi hilo katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura, Bomas of Kenya mnamo Agosti 15, 2022.
Image: ANDREW KASUKU

Shughuli ya uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 ambayo imechukua siku tano hatimaye imekamilika Jumatatu asubuhi huku Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikitarajiwa kutangaza matokeo.

Meza 15 za kufanyia uhakiki wa matokeo katika Bomas of Kenya zilikuwa tupu Jumatatu asubuhi.

Meza chache tu zilikuwa na makarani wa IEBC ambao walikuwa wanashiriki katika mazungumzo ya sauti ya chini baada ya kumaliza kazi za karatasi.

Ndani ya ukumbi wa Bomas, viti vya Azimio na Kenya Kwanza vilikuwa vimekaliwa kufikia saa tatu asubuhi.

Wajumbe na mabalozi wa kigeni pia waliketi mapema saa mbili unusu asubuhi kuashiria matangazo yanawezekana kutolewa leo.

Pia kuna uwepo mkubwa wa wanausalama katika ukumbi wa mikutano, maeneo jirani na lango kuu.

Mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio iko ukumbini zikingoja tangazo kubwa la mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.