"Hongera kaka!" Staa wa R&B Akon asherehekea ushindi wa Ruto

"Hongera sana ndugu yangu mpendwa William Ruto anapotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Kenya," Akon alisema.

Muhtasari

•Mzaliwa huyo wa Marekani kwa wazazi wa Senegal amemtambua Ruto kama kaka yake na kusherehekea ushindi wake.

•Diamond aliwahimiza Wakenya kuungana na kufanya kazi pamoja kuenda mbele licha ya tofauti zao za kisiasa.

Akon na rais mteule William Ruto.
Image: HISANI

Staa wa R&B Aliaune Damala Badara Akon Thiam almaaruufu Akon amejiunga na orodha ndefu ya watu mashuhuri ambao wamempongeza rais wa Kenya mteule William Ruto.

Katika salamu zake za pongezi, mzaliwa huyo wa Marekani kwa wazazi wa Senegal amemtambua Ruto kama kaka yake na kusherehekea ushindi wake.

"Hongera sana ndugu yangu mpendwa William Ruto anapotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Kenya,"  Akon aliandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram wenye wafuasi milioni 7.8.

Ujumbe huo ulidokeza kwamba msanii huyo maarufu anaweza kuwa na uhusiano wa karibu usiojulikana na rais mteule.

Hapo awali, staa wa Bongo Diamond Platnumz pia alikuwa ametuma salamu kwa Wakenya kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya urais.

Diamond ambaye hivi majuzi alitumbuiza katika mkutano wa mwisho wa Azimio uwanjani Kasarani aliwahimiza Wakenya kuungana na kufanya kazi pamoja kuenda mbele licha ya tofauti zao za kisiasa.

"Pongezi sana wana Kenya kwa kuhitimisha zoezi la uchaguzi na kumpata rais leo.. sasa hivi tena si Team Ruto, Wajackoyah ama Team Odinga, ni pamoja team Kenya ili kwa pamoja kuendeleza maendeleo ya Kenya na wana Kenya kwa ujumla," Bosi huyo wa WCB alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Baadhi ya viongozi wa mataifa mbalimbali hasa ya Afrika pia wametuma pongezi zao kwa Ruto baada ya kutangazwa kama rais mteule. Viongozi hao ni pamoja na rais wa Uganda Yoweri Museveni, Samia Suluhu wa Tanzania, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini,  Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Jenerali Évariste Ndayishimiye wa Burundi na waziri mkuu wa Ethiopia  Abiy Ahmed miongoni mwa wengine.