EU Yatoa Wito wa Suluhu la Amani la Mzozo wa kura ya Raila Huku Ikipongeza Uchaguzi wa utulivu

Odinga alitangaza kuwa ataelekea mahakamani kupinga matokeo hayo aliyoyataja kuwa batili

Muhtasari

•  Katika matokeo yaliyotolewa na IEBC Odinga alishindwa kwa karibu sana na mpinzani wake mkuu William Ruto.

Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya kwa Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama Josep Borrell na Waziri wa Mambo ya Nje Raychelle Omamo wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena mnamo Januari 28, 2022. Picha: MFA
Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya kwa Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama Josep Borrell na Waziri wa Mambo ya Nje Raychelle Omamo wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena mnamo Januari 28, 2022. Picha: MFA

Muungano wa Ulaya (EU) umetaka suluhu la amani na la kisheria kwa malalamishi ya mgombea urais wa Azimio La Umoja Raila Odinga kukataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kusuluhishwa kwa mzozo huo kwa njia ya utulivu na kuwataka viongozi wote wa kisiasa kuepuka ghasia na badala yake watetee amani.

“EU inazingatia matokeo ya IEBC kumtangaza Bw William Ruto mshindi wa uchaguzi na uamuzi wa kukata rufaa wa Bw Raila Odinga. Mzozo unaoendelea na tashwishi zozote zilizosalia kuhusu uchaguzi huu lazima zitatuliwe kwa amani kupitia taratibu zilizopo za kisheria," Mwakilishi Mkuu wa EU Josep Borrell alisema katika taarifa.

“Viongozi wote wa kisiasa na kijamii lazima waepuke vurugu zozote na watoe wito wa utulivu. Ni wakati wa uongozi wa kisiasa na wajibu kutoka kwa wale wote wanaohusishwa na mchakato wa uchaguzi,” aliongeza.

Borell hata hivyo aliwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani katika kipindi cha uchaguzi na akaelezea matumaini yake katika kuimarisha uhusiano kati ya serikali inayokuja ya Kenya na EU.

"Tunatazamia kufanya kazi pamoja na kujiendeleza zaidi, pamoja na uongozi wa baadaye wa Kenya, Mazungumzo ya Kimkakati ya EU-Kenya yenye manufaa kwa pande zote mbili yalianza Juni 2021."

Katika matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo Agosti 15, Bw Odinga alishindwa kwa karibu sana na mpinzani wake mkuu William Ruto baada ya kupata kura 6,942,930, ikiwa ni asilimia 48.8 ya kura zote zilizopigwa. Ruto alipata kura 7,176,141, ikiwa ni asilimia 50.49.

Lakini Jumanne alasiri, Bw Odinga alitangaza kuwa ataelekea mahakamani kupinga matokeo hayo aliyoyataja kuwa batili na kumshutumu Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kwa kukiuka Katiba na sheria za uchaguzi.

Wakati huo huo Odinga amewataka wafuasi wake kuwa watulivu, huku kikosi chake cha mawakili kikitafuta njia za kisheria kutaka tangazo la Chebukati lifutiliwe mbali mahakamani.