Uchaguzi wa Ugavana kaunti ya Mombasa na Kakamega umeahirishwa

Muhtasari
  • Uchaguzi wa Ugavana kaunti ya Mombasa na Kakamega umeahirishwa
  • mwenyekiti Wafula Chebukati alisema hii ni kutokana na kunyanyaswa kwa wafanyikazi wa tume katika Bomas of Kenya mnamo Jumatatu
akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 10, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 10, 2022
Image: ENOS TECHE

IEBC imeahirisha tena uchaguzi wa ugavana wa Kakamega na Mombasa.

Katika taarifa yake Jumatano, mwenyekiti Wafula Chebukati alisema hii ni kutokana na kunyanyaswa kwa wafanyikazi wa tume katika Bomas of Kenya mnamo Jumatatu.

"Hii imezua hofu kwa wafanyikazi ambao sasa hawawezi kuripoti afisi kazini. Unyanyasaji huu lazima ukomeshwe mara moja," Chebukati alisema.

"Kwa kuzingatia mazingira yaliyopo, Tume imeahirisha uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika tarehe 23 Agosti 2022, hadi tarehe itakayotangazwa kupitia notisi ya gazeti la serikali," Chebukati alisema.

Wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya urais, Chebukati na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu na Mkurugenzi Mtendaji Marjan Marjan walishambuliwa kimwili, kushambuliwa na kujeruhiwa na watu waliokuwa kwenye mrengo wa baadhi ya viongozi wa kisiasa.

"Tunatoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka dhidi ya wavamizi hawa bila kujali itikadi zao za kisiasa," Chebukati alisema.

Kando na uchaguzi wa ugavana wa Kakamega na Mombasa, IEBC pia ilikuwa imepanga uchaguzi katika maeneo bunge manne na wadi mbili mnamo Agosti 23 ambazo zote sasa zimefutiliwa mbali.

Haya ni eneo bunge la Kitui Vijijini katika Kaunti ya Kitui, eneo bunge la Kacheliba katika Kaunti ya Pokot Magharibi, eneo bunge la Pokot Kusini katika kaunti ya Pokot Magharibi na eneo bunge la Rongai katika kaunti ya Nakuru.

Uchaguzi wa Mbunge wa Kaunti ya Nyaki Magharibi katika eneo bunge la Imenti Kaskazini kaunti ya Meru na Kwa Njenga katika eneo bunge la Embakasi Kusini kaunti ya Nairobi pia umeahirishwa.