Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amewaandikia Wakenya ujumbe akiwataak kumuweka kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga katika maombi.
Katika kile Sonko alitaja kama ni mikosi inayomuandama, aliambatanisha video za mwanasiasa huyo mkongwe akipinga matokeo ya uchaguzi tangu mwaka 1997, 2007, 2013 na 2017 na kusema kwamba si bure yeye tu awe ndio wa kupoteza na kupinga bali huenda kuna kitu kinamuandama kama mkosi au laana.
“Wapendwa Wakenya, kwa heshima zote kwa taifa na kwa rafiki yangu Raila Amollo na licha ya yote yaliyopita na yanayoendelea sasa, nadhani ni wakati mwafaka tumweke Baba katika maombi kama nchi. Mimi binafsi nadhani katika hilo lazima kitu kitakuwa kibaya mahali fulani sababu mwaka 1997 Baba alishindwa akapinga matokeo ya uchaguzi. Mnamo 2002 sawia, 2013 na 2017 tena hali hiyo hiyo ilirudiwa,” Sonko alisema.
Sonko alizidi kusema kwamba hata uchaguzi wa mwaka huu ambao matangazo yake yamefanyika juzi kati ambapo mshindani wa Odinga, William Ruto alikabidhiwa cheti cha ushindi bado Odinga ameleta kawaida yake ya kupinga, kitu ambacho Sonko amesema si sawa bali huenda ni mazingaombwe yanaambatana nacho.
“Mimi nafikiri au kuna mtu alimroga Baba anafaa kukemewa hayo mapepo ya urogi ama ni laana. Nini unadhani; unafikiria nini?” Sonko aliwaambia Wakenya kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Matamshi haya ya Sonko yanakuja siku moja tu baada ya Odinga kuitisha mkutano wa wanahabari na kupinga matokeo ya IEBC yaliyompa Ruto ushindi na hivyo kumfanya Odinga kuingia kwenye rekodi ya kuwa mwanasiasa aliyewania urais nchini Kenya mara tano mtawalia bila kuibuka mshindi.