"Matiang'i na Kibicho muda wenu umekwisha," - Rigathi Gachagua

Aliwaambia wakome kusumbuka kumsaidia Raila kwani uchaguzi ulikamilika.

Muhtasari

• Gachagua alisema wakenya walishapiga kura na wakamaliza mchakato huo, hakuna vile Matinag'i na Kibicho watasaidia Raila kushinda.

Naibu rai mteule Rigathi Gachagua
Naibu rai mteule Rigathi Gachagua
Image: Facebook//William Ruto

Naibu rais mteule Rigathi Gachagua amesema kwamba wakenya hawatarudi kushiriki katika uchaguzi tena kwani walishamalizana na mchakato huo na kusahau kabisa.

Akizungumza Jumatano wakati wa mkutano wa muungano wa Kenya Kwanza uliondaliwa na viongozi wote walioteuliwa katika uchaguzi uliofanyika wiki jana, Gachagua alisema kwamba Wakenya sasa wanatazamia kuendeleza michakato ya kunusuru maisha yao kutoka kwa gharama inayozidi kupanda kila kukicha na katu hawatarubuniwa kurudi katika kushiriki uchaguzi tena.

Kiongozi huyo ambaye kabla kuteuliwa kama naibu rais alihudumu kama mbunge wa Mathira aliwarushia cheche Waziri wa masuala ya ndani Dkt. Fred Matiang’i na katibu wa kudumu katika wizara hiyo Karanja Kibicho na kuwaambia kwamba hakuna haja ya wawili hao kuendeleza shinikizo la kile alikitaja kuwa ni kusumbuka kumuokoa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kwani muda wao wa kuhudumu ofisini tayari umekwisha.

“Muda wa Matiang’i na Kibicho umekwisha, hakuna haja ya kushinda kusumbuka kumuokoa Raila Odinga kwani Wakenya tayari wameshapiga kura na kuwachagua viongozi wao na hawatarudi kushiriki mchakato huo,” Gachagua alinukuliwa.

Haya yanakuja siku mbili tu baada ya Odinga kudokeza kwamba muungano wake upo tayari na Ushahidi wa kutosha kuelekea mahakamani kupinga matokeo ya urasi ambayo yalimpa William Ruto ushindi kama rais mteule wa tano wa Kenya.

Muungano wa Kenya Kwanza ukiongozwa na naibu rais anayeondoka William Ruto umekuwa kwa muda mrefu ukikwaruzana mabega na baadhi ya mawaziri katika serikali ya Jubilee kwa kile wamekuwa wakisema ni mawaziri hao kutumia rasilimali za umma kuwapigia debe wanasiasa wanaoegemea upande wa rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.

Ruto amekuwa katika vita vya maneno mara si moja na Waziri Matiang’i na katibu katika wizara hiyo Kibicho huku akisema wawili hao wanatumia dola kuhangaisha wanasiasa wasioegemea mrengo wao na Jumatano rais Mteule huyo alisema kwamab licha ya vitisho vingi walivyopokea kutoka kwa baadhi ya mawaziri serikalini hatoenda kushiriki katika mchakato wa kutaka kulipiza kisasi dhidi yao.