(+video) "Usitishwe na kimya cha rais Kenyatta," Wetangula amwambia Ruto

Tunamwambia rais wetu Ruto asibabaike. - Wetangula.

Muhtasari

• "Wale ambao wametembea nawe watafanya kila liwezekanalo kibinadamu kukufanya uonekane mzuri, uonekane tofauti na kukufanya ufanikiwe,” - Wetangula kwa Ruto.

Baada ya tume ya IEBC kumtangaza rasmi William Ruto kuwa ndiye rais mteule wa Kenya, wengi wamekuwa wakisubiria kama rais anayeondoka Uhuru Kenyatta atampongeza au hata kutoa tamko lolote haswa ikizingatiwa kwamba aliweka wazi hangemkabidhi Ruto funguo za ikulu na kuwataka watu kumchagua mshinde Raila Odinga.

Kinara wa chama cha FORD-K Moses Wetangula sasa amekuwa wa hivi punde kuzungumzia kimya hicho cha Kenyatta na kumtaka Ruto kutokwazika kwa njia yoyote na ukimya wake kwani Wakenya tayari walizungumza na sauti zao zilisikika kwenye debe.

“Watu wamekuwa wakiuliza mbona rais anayeondoka amesalia kimya. Mimi nawaambia msifadhaike, kama atasema chochote ama atakuwa kimya haina maana, watu wa Kenya walishaongea kupitia debeni na sauti hiyo inatosha,” Wetangula alisema katika video moja ambayo imepakiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Akitolea mfano wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2020, Wetangula alisema rais wa zamani Donald Trump alikataa kumtambua rais wa sasa Joe Biden lakini ushindi wake ulidumishwa.

Wetangula alimtaka Ruto kutoyumbishwa na vitisho vya washindani wao kutaka kuelekea mahakamani na badala yake kumsihi aendeleze mbio zake katika kuwahudumia Wakenya kwani taifa hili limegonjeka kwa muda mrefu kutokana na siasa.

“Washindani wetu wanaostahili wanatishia kwenda mahakamani lakini umeona wanachosema kimejaa makosa rahisi na ya bei nafuu ya hesabu na sheria. Tunamwambia rais wetu asibabaike. Weka macho yako kwenye mpira, tumikia watu wa Kenya. Wale ambao wametembea nawe watafanya kila liwezekanalo kibinadamu kukufanya uonekane mzuri, uonekane tofauti na kukufanya ufanikiwe,” seneta huyo wa Bungoma alimhakikishia rais mteule William Ruto.