Naibu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Juliana Cherera amekana kuwa mtumizi wa mitandao ya kijamii.
Cherera ambaye amekuwa gumzo katika siku kadhaa zilizopita tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo Jumatatu amezipuuzilia mbali akaunti nyingi za Twitter na Facebook ambazo zimeibuka na jina lake zikidaiwa kuwa zake.
Akizungumza na Citizen Digital, makamu mwenyekiti huyo wa IEBC aliweka wazi kuwa akaunti zote zinazodaiwa kuwa zake ni ghushi na kubainisha kuwa hata amezichukulia hatua.
"Sipo kwenye mitandao ya kijamii. Akaunti zote hizo za Facebook/Twitter ni fake na nimeripoti kwa mashirika/mamlaka husika,” Cherera alisema.
Haya yanajiri huku kukiwa kumezuka akaunti nyingi za Twitter na Facebook zenye jina lake ambazo zimekuwa zikichapisha jumbe tatanishi na kuonekana kutoa taarifa kuhusu mgawanyiko katika tume.
Hivi majuzi, moja ya akaunti kwenye Twitter ambayo iliaminika kuwa yake hivi iliwasihi Wakenya kukoma kuchapisha picha zake akiwa na viongozi wa Azimio wakidai kuwa wanafanya kazi pamoja.
“Mimi na wenzangu tumeonyesha ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa kujumlisha kura za Rais. Si haki kubinafsisha masuala. Picha za mimi nikitekeleza majukumu katika nafasi yangu ya awali hazina uhusiano wowote na ukweli tuliouweka wazi,” Chapisho lilisoma.
Siku ya Jumatatu, Cherera aliwaongoza makamishna wengine watatu wa IEBC kujitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais hata kabla ya kutangazwa na mwenyekiti wa tume Wafula Chebukati.
Cherera kwa pamoja na Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya walidai kuwa hawakuridhishwa na jinsi hatua ya mwisho ya uchaguzi ilivyoendelezwa na kwa hiyo hawangeweza kumiliki matokeo hayo.
"Tumefanya uchaguzi wa 2022 kwa njia bora zaidi. Tumehakikisha kuwa tumeboresha viwango. Tumefanya kazi nzuri lakini baadhi ya mambo yanahitaji kuwekwa wazi.Tupo hapa kwa sababu ya hali ya kutoeleweka ambayo hatua ya mwisho ya uchaguzi mkuu huu. Hatuwezi kuchukua umiliki wa matokeo ambayo yanaenda kutangazwa," Walisema katika kikao na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena.