Miguna amtuhumu waziri wa ICT kutumiwa na Azimio kudukua fomu 34A za IEBC

Miguna alimzomea Joe Mucheru kwa kusema kwamba anatumiwa na Azimio ili kubadilisha fomu 34A kwenye wavuti wa IEBC.

Muhtasari

• Miguna aisema kwamba Mucheru anatumika ili kubadilisha fomu hizo ili kuweka zile zenye takwimu za kumpendelea Raila.

Waziri wa ICT Joe Mucheru wajibizana na wakili Miguna Miguna kuhusu fomu 34A katika wavuti wa IEBC
JOE MUCHERU, MIGUNA MIGUNA Waziri wa ICT Joe Mucheru wajibizana na wakili Miguna Miguna kuhusu fomu 34A katika wavuti wa IEBC
Image: Twitter

Mwanasheria Miguna Miguna katika siku za hivi karibuni ameibuka kuwa mtetezi nguli wa sera za rais mteule William Ruto huku akimsuta vikali kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2017 alikuwa mwandani wake mpaka kumuapisha kama rais wa watu Januari 2018.

Miguna sasa anaibua madai kupitia mtandao wa Twitter kwamba Waziri wa utandawazi na mawasiliano Joe Mucheru amekuwa akishirikiana na muungano wa Azimio kuzifuta fomu 34A kutoka wavuti wa tume ya IEBC baada ya mrengo huo kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyomtaja naibu rais anayeondoka William Ruto kama mshindi wa urais.

“Azimio wanatumia mtaalam wa IT wa @IEBCKenya aliyetekwa nyara na walaghai wa ICT wa China walioajiriwa na @mucheru kufuta fomu 34As na kuingiza fomu zao ghushi 34A zenye takwimu za RAO zilizoimarishwa ili Mahakama ya Juu imtangaze rais mteule wa RAO. Ijulikane na Wazalendo,” Miguna Miguna aliibua madai hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Baada ya kuibua madai haya, Waziri Mucheru alishindwa kustahimili vishindo vya jinsi jina lake lilikuwa linatajwa hovyo na kuamua kujibu mipigo kwa kuwataka mawakili hao Miguna Miguna na Ahmed Nasir kukoma kumtaja na badala yake kushughulika na kesi ambayo Azimio itawasilisha katika mahakama ya upeo wa juu Jumatatu adhuhuri.

“Nadhani wanasheria @MigunaMiguna Na @ahmednasirlaw wanapaswa kushikamana na taaluma yao. Kila mara @mucheru Hii @mucheru ile, huna mawakili wako wa kushughulikia? Ni siku yako kuu katika Mahakama ya Juu kesho, zingatia! au mtakuwa watazamaji kama mimi?” Waziri Mucheru alicharuka kwa hasira.

Aidha, Miguna Miguna hakukomea hapo kwani alimjibu vikali Waziri Mucheru huku akimwambia kwamba haogopi na akitaka anaweza enda na akamripoti kwa rais anayeondoka, Uhuru Kenyatta.

“Bw Joe Mucheru: Unashikilia afisi ya umma ambayo unaitumia vibaya na kuihujumu Katiba. Walipakodi wa Kenya wanakulipa ili kudumisha Katiba. Nimejitolea kuwafichua, kupigana na kuwashinda wafanyabiashara wa kutokujali kama wewe - bila msamaha. Nenda ukamwambie dhalimu Uhuru Kenyatta kwamba,” mwanasheria Miguna alijibu.