IEBC imetangaza Agosti 29 kuwa siku ambayo itaendesha uchaguzi mdogo katika maeneo ambayo upigaji kura uliahirishwa katika Uchaguzi Mkuu uliokamilika.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume hiyo imejitayarisha kikamilifu kuandaa uchaguzi Jumatatu baada ya kuahirisha zoezi hilo mara mbili.
"Tutafanya uchaguzi Jumatatu isipokuwa kutakuwa na mapendekezo mengine kutoka kwenu," Chebukati aliwaambia wagombeaji walioshiriki uchaguzi huo wakati wa mkutano nao katika eneo la Bomas of Kenya, Nairobi.
Makamishna wote saba wa IEBC walihudhuria mkutano huo. Mwaniaji ugavana wa Kakamega Cleophas Malala alisema hawana tatizo na tarehe iliyopendekezwa na tume hiyo.
"Hata hivyo tunataka kujua kama kutakuwa na muda na fedha za kutosha kwa ajili ya elimu ya uraia. Wapiga kura wetu wanahitaji kufahamishwa kuhusu tarehe na kuhimizwa kujitokeza kwa ajili ya zoezi hilo," Malala alisema.
IEBC ilisimamisha mara mbili uchaguzi wa ugavana wa Mombasa na Kakamega na viti vinne vya maeneo bunge - Pokot Kusini, Kitui Vijijini, Rongai na Kacheliba.
IEBC ililazimika kuahirisha uchaguzi katika kaunti za Kakamega na Mombasa kufuatia mkanganyiko wa karatasi za kupiga kura ya ugavana katika kaunti hizo ambapo karatasi tofauti zilisambazwa kwenda huko siku moja kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 kufanyika.
Kuahirishwa kwa uchaguzi huo haswa wa ugavana Mombasa na Kakamega kumeibuka kuwa jambo la kupigiwa siasa baina ya mirengo miwili hasimu huku wagombea wanaoegemea mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya wakitaka uchaguzi huo kuendelea jinsi ulivyoratibiwa Jumanne wiki hii huku wale wanaoegemea Kenya Kwanza wakionekana kutokuwa na tashwishi kuhusu kusogezwa mbele kwa tarehe husika.
Wiki jana Chebukati alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa kutaja sababu za kiusalama kwa maafisa wanaosimamia chaguzi hizo, baada ya kusema kwamba maafisa wa IEBC walijeruhiwa katika ukumbi wa Bomas huku pia afisa mmoja katika eneo bunge la Embakasi East akitoweka na kishaq mwili wake kupatikana Loitoktok siku chache baadae.