Huku wimbi la wanasiasa nchini Kenya wakionekana kuwa na uchu wa kujiegemeza na upande wa serikali ijayo ambayo tayari tume ya uchaguzi na mipaka IEBC imemtangaza William Ruto licha ya ushindi wake kupingwa mahakamani na mshindani wake Raila Odinga, wanasiasa wengi waliokuwa mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya wameendelea kuhama na kujiunga na mrengo wa Ruto.
Wiki jana, vyama na wanasiasa wengi waliokuwa ndani ya muungano wa Azimio pamoja na wale waliokuwa wakigombea kwa tikiti huru walijiunga na Ruto huku suala hilo likizua tumbo joto miongoni mwa wana Azimio waliosema ni njama ya Ruto kusambaratisha Azimio.
Sasa Ruto ameendeleza kutupa ndoana yake katika baadhi ya viongozi tajika waliokuwa Azimio na ndoana yake safari hii imemnasa gavana anayeondoka wa Makueni msomi wa sheria Kivutha Kibwana ambaye amejiunga Kenya Kwanza.
Akimkaribisha katika makazi yake rasmi huko Karen, Ruto alisema kwamba Kibwana na viongozi wengine kutoka kaunti ya Makueni sasa ni rasmi miongoni wa timu kubwa ya Kenya Kwanza na kudokeza kwamba msomi huyo wa sheria sasa atajiunga katika timu ya mawakili watakaotetea ushindi wa Ruto katika mahakama ya upeo kwenye kesi ambayo iliwasilishwa jana na muungano wa Azimio la Umoja.
"Gavana wa Makueni atajiunga na timu ya wanasheria wa Kenya Kwanza katika ombi linaloendelea la kupinga uchaguzi wa urais. Katika Makazi ya Karen, nimemkaribisha Gavana Kibwana mrengo wa Kenya Kwanza akiandamana na viongozi wengine," Ruto alidokeza kwenye Facebook yake.
Aidha, naibu rais huyo anayeondoka alisema kama Kenya Kwanza wanajivunia maendeleo ambayo gavana huyo ametekeleza katika kaunti hiyo kwa muda wake wa miaka kumi ofisini.
"Tunashirikiana na uongozi ambao Prof. Kivutha Kibwana amedhihirisha kwa kukubali kufanya kazi nasi katika kuendeleza ajenda ya maendeleo ya nchi yetu," Ruto alisema.
Wiki jana viongozi kadhaa waliogombea kwa tikiti huru kama vile gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza walijiunga kwenye kambi ya Ruto huku pia chama cha UDM kikiongozwa na kiongozi wake Ali Roba ambaye ni seneta mteule wa Mandera walijiunga Kenya Kwanza pia.