Mzozo wa vita vya ubabe katika chama cha Roots unazidi kuchuua mikondo tofauti ya kupinda kila uchao, huku sasa ikiwa ni wazi kabisa kwamba kinara wa chama hicho wakili msomi George Wajackoyah na aliyekuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 Justina Wamae hawala tena kutoka sinia moja.
Jana, uongozi wa chama hicho ulimuandikia barua ya malalamishi Wamae kwa kile waliteta kwamba mgombea mwenza huyo kwa mara kadhaa katika mitandao ya kijamii na pia kwenye vyombo vya habari amekuwa akitoa matamshi yanayokinzana na kanuni za chama hicho na hivyo kumtaka kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama kujitetea dhidi ya shtuma hizo.
Barua hiyo ilikuwa ikilalama kwamba Wamae alimpongeza rais mteule William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua pasi na kushauriana na uongozi wa chama chake ambao walikuwa ni washindani katika kinyang’anyiro cha urais uliokamilika majuma mawili yaliyopita.
Walisema kwamab kauli za Wamae zinahitilafiana na mienendo ya chama na pengine kuchukuliwa kama kauli za chama jambo ambalo linachafua picha ya chama cha Roots na hiyo ndio sababu kuu ya kumtaka kufika mbele ya kamati ya nidhamu kukabiliana na maswali dhidi ya hulka hizo zake.
Barua hiyo pia ilitaja baadhi ya vitu ambavyo wamemkabidhi Wamae katika miezi miwili ambayo amekuwa kama mwanachama vikiwemo makazi na gari la kusafiria, suala ambalo Wamae pia aliligusia katika jibu lake kupitia Twitter.
Sasa Wamae ambaye hajatulia kabisa kupungwa na upepo huo wa chama cha Roots ametema moto huku akitaja barua hiyo inayomtaka kufika mbele ya kamati ya nidhamu kuwa ya hovyo na kuapa kamwe hatohudhuria kikao hicho alichoamrishwa kufika tarehe 26 Agosti.
“Sitajibu ujinga. Lakini kwenye malazi na gari ambalo unadhani kwamba 'umenisaidia' unaweza kuliondoa katika NDOTO zako. Ni chama chako fanya unachoona kinafaa, nitazidi kusonga mbele kama mwanajeshi,” Wamae alijibu kupitia ukurasa wajke wa Twitter.
Mgogoro wa wawili hao ulianza baada ya Wamae kumtuhumu Wajackoyah kwamba anamuunga mkono kisiri mgombea wa Azimio la Umoja Raila Odinga huku naye akitishia kujitupa nyuma ya William Ruto wa Kenya Kwanza.