Wahuni walijaribu kushambulia maafisa wetu wanaoshughulikia rufaa - IEBC

Wafanyakazi hao walikuwa wakitayarisha majibu ya malalamishi ya uchaguzi wa urais yaliyowasilishwa Jumatatu.

Muhtasari

•Kulingana na taarifa  iliyotolewa na tume hiyo, jaribio hilo lilitokea mwendo wa saa mbili unusu usiku katika jumba lililo Nairobi.

•IEBC imemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kuhakikisha kuwa wafanyikazi wake wanalindwa.

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Image: ENOS TECHE

Jumatatu genge la wahuni waliokuwa wamebeba silaha walidaiwa kujaribu kuwashambulia wafanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kulingana na taarifa  iliyotolewa na tume hiyo, jaribio hilo lilitokea mwendo wa saa mbili unusu usiku katika jumba lililo Nairobi.

Wafanyakazi hao walikuwa wakitayarisha majibu ya malalamishi ya uchaguzi wa urais yaliyowasilishwa mapema siku hiyo.

IEBC ilisema kundi hilo la wahuni  lilifukuzwa na walinzi ambao walikuwa wamesimamia  eneo hilo.

"Kundi lililopangwa la wahuni waliokuwa na silaha chafu walijaribu kushambulia wafanyikazi wa IEBC wakitayarisha majibu ya malalamiko ya uchaguzi wa Rais katika jumba la Nairobi. Hata hivyo, walizuiwa na walinzi," Tume ilisema.

IEBC imemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kuhakikisha kuwa wafanyikazi wake wanalindwa.

"Tume inalaani kitendo hiki cha uhuni na vitisho, na inamtaka Inspekta wa Polisi (IG) kukomesha matumizi mabaya haya ya wazi ya Utawala wa Sheria."

Haya yalijiri huku afisa msimamizi wa IEBC wa eneo bunge la Gichugu Geoffrey Gitobu akiripotiwa kuaga dunia  baada ya kuugua kwa njia ya kutatanisha na kuzimia akiwa katika afisi ya IEBC ya Nanyuki siku ya Jumatatu.

Afisa huyo alikuwa ameenda kuiona familia yake Nanyuki wikendi baada ya zoezi kali la uchaguzi na alitakiwa kurejea Kirinyaga Jumatatu ili kujiandaa kurejea kazini baadae wiki hii.

msimamizi wa uchaguzi wa kaunti ya Kirinyaga Jane Gitonga alisema kuwa mzee huyo wa miaka 57 hajawahi kulalamika kuhusu ugonjwa wowote na kwa hivyo uchunguzi wa maiti ungefanywa ili kubaini chanzo cha kifo.