Muungano wa Azimio - One Kenya unaoongozwa na Raila Odinga umeanzisha mikakati ya kuwarejesha wanachama ambao walibadili uaminifu wao na kuungana na Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi wa maspika wa bunge la kitaifa na seneti.
Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema wameanza kuwahusisha wale ambao wametangaza kumuunga mkono Rais mteule William Ruto kabla ya kikao cha kwanza cha wabunge hayo.
“Unadai aje kuchukua wanachama wetu ambao Odinga aliwafanyia kampeni binafsi na kupigiwa kura na watu wengi,?” Mbadi alisema.
Muungano huo ulifanya mkutano wa mikakati huko Upper Hill siku ya Ijumaa, ambapo umuhimu wa Spika wa Bunge la Kitaifa ulisisitizwa.
Jumanne iliyopita, wabunge hao waliunda kamati ambayo itasimamia ugavi wa nyadhifa za uongozi wa bunge miongoni vyama tanzu.
Wanachama wa kamati hiyo ni Opiyo Wandayi (Ugunja), Makali Mulu (Kitui Kati), Adan Keynan (Eldas), Yusuf Haji (Kamukunji), Naisula Lesuuda (Samburu Magharibi), Danson Mwashako (Wundanyi), Abdisabir Shuriye (Mbalambala), Julius Mawathe (Embakasi Kusini), John Mbadi na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo.
Wawakilishi wa maeneo mbalimbali wanatakiwa kupendekeza majina ya watu wanaofaa kuwania nafasi hizo.
Watu hao watahojiwa kabla ya kuwasilisha yule mgombea mmoja ambaye anapendekezwa kwa nafasi hiyo.
Lengo ni kuwasilisha mwagombeaji wa wenye uwezo wa kushawishi uungwaji mkono.
Kulingana na sheria mgombeaji wa wadhifa wa spika lazima aungwe mkono na angalau thuluthi mbili au 233 kati ya wabunge 349 wa Bunge la Kitaifa katika awamu ya kwanza au yule atakayeshinda kwa wingi wa kura katika awamu ya pili.