''Nawatakia heri njema'' Lee Kinyanjui hatimaye akubali kushindwa na Susan Kihika

Kinyanjui alikosa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Kihika kama gavana mpya wa Nakuru.

Muhtasari

•Kinyanjui alitoa shukrani kwa wakazi wa Nakuru kwa kumpatia fursa nzuri ya kuwahudumia  kama gavana wao wa pili.

•Kinyanjui alisema kuwa  kuna haja kubwa kwa Wakenya kuungana mkono katika ujenzi wa taifa kufikia  ustawi.

Gavana wa Nakuru Lee KInyanju
Image: MAKTABA

Aliyekuwa gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui hatimaye  amekubali kushindwa katika kinyanganyiro cha ugavana wa kaunti hiyo.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, Kinyanjui alitoa shukrani kwa wakazi wa Nakuru kwa kumpatia fursa nzuri ya kuwahudumia  kama gavana wao wa pili.

"Kwa maisha, mwanzo wa jambo moja huashiria mwisho wa jambo lingine. Imekuwa fahari kubwa kuwahudumia wenyeji wa Nakuru kama gavana wao, ninawatakia wakaazi wa Nakuru kila la heri," Alisema Kinyanjui.

Mwanasiasa huyo alidokeza kuwa, hakuna kinachomfurahisha zaidi kuliko kuona kaunti ya Nakuru ikiwa na maendeleo na amani. 

"Nawashukuru watu wote waliotembea nami katika safari hiyo. Kuanzia wafanyakazi, bunge la kaunti hadi washirika wa nje, mchango wenu unathaminiwa sana. Tunasherehekea uzalendo wenu," aliongeza.

Kinyanjui alisema kuwa  kuna haja kubwa kwa Wakenya kuungana mkono katika ujenzi wa taifa kufikia  ustawi.

''lazima sote tuendelee kulijenga taifa letu kwa manufaa ya kizazi kijacho Mungu ibariki Nakuru. Asante," alisema bosi huyo wa kaunti anayeondoka.

Mnamo Jumatano, Agosti 25, Kinyanjui alikosa hafla ya kuapisha Susan Kihika kama gavana mpya wa Kaunti hiyo.

Naibu wa Kinyanjui Erick Korir hata hivyo alihudhuria hafla hiyo.

Kihika alikuwa akiwania kiti cha ugavana wa Nakuru kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) na alitangazwa mshindi baada ya kuzoa kura 440,707 dhidi ya 225,623 za Kinyanjui.